Reli mpya imejengwa, usafiri umeanza

NA LWAGA MWAMBANDE

JUNI 14,2024 Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza kutoa huduma za kibiashara kupitia Reli ya Umeme ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.
"Hii ni hatua kubwa katika miundombinu ya usafiri ya Tanzania inayotarajia kuboresha uunganishaji na ufanisi na kuchochea ukuaji wa uchumi," alisema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli la Tanzania, Masanja Kadogosa.

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alisema abiria 1,400 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro walisafiri katika treni ya kwanza ya umeme ya SGR bila malipo, na kuongeza kuwa treni iliondoka Dar es Salaam saa 12:10 asubuhi na kufika Morogoro saa 1:55 asubuhi.

"Shughuli za kibiashara za kwanza za umeme za SGR kati ya maeneo hayo mawili zilikuwa za kihistoria," alisema Kihenzile, na kuongeza kuwa nauli za kutoka na kurudi Dar es Salaam zililipwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kama shukrani yake kwa uzinduzi wa shughuli za kibiashara.

Wakati huo huo, Kadogosa alisema mradi mzima wa SGR utakuwa na urefu wa kilomita 1,596, ukiwa na sehemu tano, kutoka Dar es Salaam hadi mkoani Mwanza.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande amesema,mafanikio haya ni hatua njema za kuharakisha maendeleo si tu kwa wananchi na pia kwa Taifa. Endelea;

1:Walisema halianzi, sasa mbona limeanza,
Hapa ni kupanda ngazi, wenye macho twajifunza,
Mambo haya yako wazi, kumbukumbu tunatunza,
Ni treni la mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

2:Inayopewa maua, na kupaswa kuitunza,
Ni Serikali twajua, na kiongozi wa kwanza,
Rais tunamjua, utendaji atufunza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

3:Muda ni mfupi huo, kufika toka kuanza,
Sasa tuna machaguo, muda wetu kuutunza,
Barabara reli chuo, kama kidato cha kwanza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

4:Heko Rais Samia, treni umeme kuanza,
Dare-Moro kuanzia, twafurahi kwa machenza,
Na Dodoma kufikia, baadaye hadi Mwanza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

5:Nchi ulipochukua, na Urais kuuanza,
Yako tuliyachukua, pale Dodoma si Mwanza,
Ya kwamba hutatangua, miradi aliyoianza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

6:Kazi yako twaiona, wamaliza alianza,
Reli mpya twaiona, usafiri umeanza,
Na kwingine tunaona, ni ujenzi hadi Mwanza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

7:Sasa ‘miradi’ mitatu, kula matunda twaanza,
Rais unafanya tu, kumbukumbu tunatunza,
Twapokea roho kwatu, uongozi twajifunza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

8:Reli mpya imejengwa, usafiri umeanza,
Bwawa umeme kujengwa, matumizi yameanza,
Dodoma yazidi jengwa, Serikali kuitunza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

9:Kauliyo umeshika, toka kazi kuianza,
Wazidi kuchakarika, kumaliza aloanza,
Na ya kwako yaibuka, nchi kuzidi itunza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro

10:Kichobaki matumizi, haya tuliyoanza,
Hapa tusema kwa wazi, tusije tukajiponza,
Yawe mema matumizi, utunzaji twajifunza,
Ni treni mwendokasi, Dasalamu-Morogoro.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news