NA LWAGA MWAMBANDE
KWA mujibu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, miili yetu ina chembechembe hai nyingi ambazo huzaliana, hukua na kufa kwa mpangalio maalum.
Picha na The Sun.
Chembechembe hizi zinapobadilika na kuanza kuzaliana na kukua katika utaratibu ambao sio wa kawaida ndio zinasababisha saratani.
Aidha,chembe chembe za saratani hufuata mfumo huo usio wa kawaida na zinazaliana haraka zaidi bila mpangilio na kukua kwa haraka,wakati mwingine kuwa na umbile kubwa zaidi.
Chembechembe hizi za saratani zisipodhibitiwa mapema zina uwezo wa kusambaa na kuota sehemu nyingine ya mwili wa mhusika.
Vile vile, saratani inatajwa kuwa ni uvimbe unaojitiokeza mahala popote katika mwili wa binadamu, uvimbe huu hauna maumivu yoyote mwanzoni.
Saratani zipo za aina nyingi na majina yake hutegemea kiungo kilichougua na aina ya chembechembe hai zilizoshambuliwa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyopo mkoani Dar es Salaam, Frank Ruta amesema bado kuna umuhimu kwa jamii kupatiwa elimu zaidi ya uelewa kuhusu ugonjwa wa saratani ambao umekuwa ukisababisha vifo vya watu wengi nchini.
Akizumgumza wakati wa mjadala wa mapambano dhidi ya saratani,Dkt.Frank amesema, ugonjwa huo unazidi kuwa tishio nchini kutokana na takwimu kuonesha wagonjwa wanaongezeka siku hadi siku.
Dkt. Frank ameishauri jamii kuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara kujua kama wana ugonjwa wa saratani ama la, ikiwa ni sehemu ya mapambano ya ugonjwa huo unaoonekana kuwa bado tishio hasa kwa wanawake.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kila mmoja anapaswa kufuata miongozo na taratibu za kiafya kutoka kwa wataalam wa afya ili kuepuka ugonjwa huo hatari.Endelea;
1:Saratani ni tishio, wala haijatoweka,
Gonjwa laleta kilio, wagonjwa waongezeka,
Elimu kwa watu ndio, njia ya kudhibitika,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
2:Elimu ikizidishwa, tatizo kueleweka,
Na watu wakafundishwa, kugundua kuepuka,
Sisi sote tutakoshwa, wagonjwa wakipunguka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
3:Daktari bingwa huyu, kansa inoeleweka,
Asema mdudu huyu, anazidi ongezeka,
Ni kweli siyo ubuyu, takwimu zinasomeka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
4:Kuna mambo ya muhimu, twapaswa kuwajibika,
Kupima afya muhimu, mara kwa mara hakika,
Kujua kansa yadumu, ama tumeiepuka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
5:Kama tunapima afya, dalili zikaoneka,
Za saratani si chafya, tiba yaweza fanyika,
Mwisho unaoogofya, tukaweza uepuka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
6:Mengine nyongeza yangu, yale yanaeleweka,
Gonjwa hili ndugu zangu, kuwahi ni kutibika,
Gundulika wanguwangu, tiba iweze fanyika,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
7:Wapo mashuhuda wengi, ambao yaliwafika,
Zile jitihada nyingi, kuwahi kukihusika,
Wameshinda goli nyingi, mwilini umekauka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
8:Mungu pia ahusika, yote yanayotufika,
Ni budi kumkumbuka, kulala na kuamka,
Mengine yalofichika, afanya yakaibuka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa
9:Umekwenda sipitali, vipimo vimehusika,
Ukaambiwa dalili, kansa kama yaibuka,
Wala usiwe dhalili, kwamba ndiyo wakatika,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
10:Kliniki kimbilia, uwakute wahusika,
Kile watakuambia, kitakwacho kufanyika,
Hicho ndicho shikilia, unaweza kuponyeka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
11:Na mimi kanikumbusha, kwenda pima nahusika,
Ndiko kupenda maisha, na mwili kujikumbuka,
Tusibaki twajichosha, kwa makubwa kuumuka,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
12:Nawaasa wanawake, sana hili mwahusika,
Wanaume msideke, kupima mnahusika,
Gonjwa hili lipunguke, kwa afya kuimarika,
Daktari Frank Ruta, ndiye huyo atuasa.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602