Sekta binafsi ilivyoshiriki kuinua mitaji ya Watanzania 2023

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema, mwaka 2023, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka na kufikia shilingi trilioni 32.06 kutoka shilingi trilioni 27.4 mwaka 2022 sawa na ukuaji wa asilimia 17.1 ikilinganishwa na lengo la asilimia 16.4.

Ukuaji huo ulitokana na maboresho katika mazingira ya biashara na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ameyasema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.

Amesema,katika kipindi hicho, mikopo katika sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 43.5 kutokana na matokeo ya hatua za kisera zilizochukuliwa Julai 2021 zilizolenga kuongeza mikopo na kushusha viwango vya riba katika sekta ya kilimo.

Aidha, mikopo katika sekta ya uchimbaji madini ilikua kwa asilimia 36.4, ujenzi asilimia 23.5 na mikopo kwa shughuli binafsi asilimia 18.1.

Kwa upande mwingine,Prof. Mkumbo amesema, sehemu kubwa ya mikopo iliendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi ikihusisha biashara ndogo na za kati sawa na asilimia 38.2 ya mikopo yote.

"Ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 14, kilimo asilimia 10.4 na viwanda asilimia 9.8."

Wakati huo huo amesema, mwaka 2023, amana za benki za biashara zilifikia shilingi trilioni 36.5 kutoka shilingi trilioni 31,429.4 mwaka 2022 sawa na ukuaji wa asilimia 16.1.

Amesema, ukuaji huo ulichangiwa na ongezeko la huduma za uwakala wa benki na matumizi ya mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma za fedha.

Katika kipindi hicho, amesema amana za sekta binafsi zilifikia shilingi trilioni 35.34 sawa na asilimia 96.8 ya amana zote kutoka shilingi trilioni 30.7 mwaka 2022.

Hadi Desemba 2023, uwiano wa amana za fedha za kigeni kwa amana zote ulifikia asilimia 25.6 kutoka asilimia 24.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Kuhusu mwenendo wa viwango vya riba, Prof. Mkumbo amesema,mwaka 2023, wastani wa riba ya jumla katika soko la fedha baina ya mabenki ulifikia asilimia 5.37 ikilinganishwa na asilimia 4.53 mwaka 2022.

Aidha, riba ya jumla ya dhamana za Serikali za muda mfupi ilifikia asilimia 7.32 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 4.64 mwaka 2022.

Mwaka 2023, Serikali kwa kushirikiana na wadau iliendelea na jitihada za kuboresha mazingira ya biashara kwa lengo la kuhamasisha benki na taasisi za fedha kupunguza na kuweka viwango rafiki vya riba za mikopo na hivyo, kuwezesha wananchi wengi kupata na kufikia huduma rasmi za kifedha.

Katika kipindi hicho, viwango vya riba za mikopo vilipungua kwa kasi ndogo ambapo wastani wa riba za jumla za mikopo ulikuwa asilimia 15.75 ikilinganishwa na asilimia 16.18 mwaka 2022.

"Viwango vya riba za mikopo ya mwaka mmoja vilipungua na kufikia wastani wa asilimia 16.53 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 16.79 mwaka 2022.

"Aidha, wastani wa riba za amana za muda maalum ulipungua hadi asilimia 7.07 mwaka 2023 kutoka asilimia 7.11 mwaka 2022.

"Kwa upande mwingine, wastani wa riba za amana za mwaka mmoja uliongezeka na kufikia asilimia 8.65 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 8.53 mwaka 2022.:

Amesema,kutokana na mwenendo huo, tofauti kati ya viwango vya riba za mikopo ya mwaka mmoja na riba za amana za mwaka mmoja ilipungua kufikia wastani wa asilimia 7.88 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 8.26 mwaka 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news