Sekta ndogo ya fedha yazidi kuimarika nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo amesema, sekta ndogo ya fedha nchini imeendelea kuimarika.
Ameyasema hayo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.

"Mwaka 2023, Benki Kuu ilipokea maombi ya leseni 2,221 kutoka kwa watoa huduma ndogo za fedha daraja la pili, ambapo watoa huduma 1,579 walipata leseni ikilinganishwa na maombi 1,558 na leseni 1,095 zilizotolewa mwaka 2022.

"Katika kipindi hicho, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ilipokea maombi ya leseni 1,215 ya watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la tatu ambapo leseni 884 zilitolewa ikilinganishwa na maombi 1,117 na leseni 759 zilizotolewa mwaka 2022."

Aidha, amesema maombi 49,026 ya watoa huduma za fedha wa daraja la nne yalipokelewa na vikundi 48,284 vilisajiliwa mwaka 2023 ikilinganishwa na maombi 37,282 na vikundi 34,127 vilivyosajiliwa mwaka 2022.

Prof.Mkumbo amesema,maombi yaliyokataliwa yalitokana na kutokidhi vigezo vya daraja husika kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo katika sekta ya huduma ndogo za fedha.

Kuhusu,Huduma Jumuishi za Fedha amesema,kwa mujibu wa Taarifa ya Utafiti wa FinScope ya mwaka 2023, kiwango cha upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha na bidhaa kiliongezeka hadi asilimia 76 na asilimia 89 mwaka 2023 kutoka asilimia 65 na asilimia 86 mtawalia mwaka 2017.

"Hii ilitokana na kasi ya ukuaji wa sekta ya fedha uliochagizwa na ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia katika kuunda na kusambaza huduma na bidhaa za kifedha.

"Uwepo wa wigo mpana wa upatikanaji wa huduma na bidhaa rasmi za fedha uliwezesha watu binafsi na jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao."

Pia amesema,mwaka 2023, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha iliandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (2023-2028).

Ni mpango unaolenga kuongeza kasi na kupanua wigo wa upatikanaji wa bidhaa na matumizi ya huduma rasmi za fedha hadi asilimia 95 na asilimia 85 ifikapo mwaka 2028 kutoka asilimia 89 na asilimia 76 mtawalia mwaka 2023.

Amesema,katika kipindi hicho, Muundo wa Mawasiliano wa Masuala ya Huduma Jumuishi za Fedha uliandaliwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news