Sekta ya Benki inavyozidi kuwa chaguo muhimu kwa Watanzania

NA GODFREY NNKO

HADI Desemba 2023, idadi ya benki ilifikia 44 kutoka benki 45 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ameyasema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.

Kupungua kwa idadi ya benki kulitokana na kuhamishwa kwa mali na madeni ya Yetu Microfinance Bank Plc kwenda NMB Bank Plc.

Aidha, matawi ya benki yaliongezeka na kufikia 1,011 mwaka 2023 kutoka matawi 998 mwaka 2022.

"Hadi Desemba 2023, amana za wateja zilifikia shilingi bilioni 37,980.8 (shilingi trilioni 37.98) kutoka shilingi bilioni 32,526.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 16.8."

Kwa upande mwingine, mikopo kwa wateja ilifikia shilingi bilioni 33,194.4 kutoka shilingi bilioni 27,309.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 21.6.

"Mwaka 2023, benki 31 zilitoa huduma za benki kwa njia ya uwakala ikilinganishwa na benki 28 mwaka 2022.

"Aidha, idadi ya mawakala wa benki iliongezeka kwa asilimia 41.1 na kufikia mawakala 106,176 mwaka 2023 kutoka mawakala 75,238 mwaka 2022."

Amesema,ongezeko hilo lilichangiwa na hatua ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendelea kulegeza masharti ya usajili wa mawakala wa benki ikiwemo kuondoa sharti la kutoa huduma za fedha kwa njia ya uwakala wa benki kwa kipindi cha miezi 18.

Ni ili kupata leseni ya kuwa wakala wa benki ambapo kwa sasa sharti ni kuwa na kitambulisho cha Taifa.

Waziri amefafanua kuwa, katika mwaka huo uwiano wa mtaji halisi na mtaji mkuu kwa mali hatarishi ulikuwa asilimia 17.7 na asilimia 18.4 ikilinganishwa na asilimia 18.0 na asilimia 18.9 mtawalia katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Aidha, uwiano wa ukwasi katika benki ulipungua hadi asilimia 28.7 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 29.4 mwaka 2022.

Hii ilitokana na sekta ndogo ya benki kuendelea kuwa thabiti na kuongezeka kwa imani ya wananchi.

Katika mwaka huo, pia kiwango cha mikopo chechefu kilipungua na kufikia wastani wa asilimia 4.3 ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2022.

Amesema,kupungua kwa mikopo chechefu kulitokana na hatua mbalimbali zilizoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania zikiwemo kuongeza ufuatiliaji wa utoaji mikopo na kuwaondoa wafanyakazi wa benki wasio waaminifu.

Vile vile kuzielekeza benki kutumia ripoti za mikopo kutoka kwa kampuni za kuchakata na kutunza kumbukumbu za mikopo.

Nyingine ni utekelezaji wa kanuni za kuwalinda walaji wa huduma za fedha za mwaka 2019 kwa kuhakikisha utunzaji wa haki na usawa kwa wakopaji.

Sambamba na kuzitaka benki na taasisi za fedha kuimarisha taratibu za utoaji na ufuatiliaji wa mikopo.

Aidha, idadi ya taasisi zilizotumia kanzidata ya wakopaji iliongezeka na kufikia 181 mwaka 2023 ikilinganishwa na taasisi 166 mwaka 2022.

"Vile vile, idadi ya wakopaji waliosajiliwa kwenye Kanzidata ya Wakopaji iliongezeka na kufikia 8,134,863 ikilinganishwa na wakopaji 5,035,031 mwaka 2022,"amesema Prof.Mkumbo.

Wakati huo huo amesema, mwaka 2023, Benki Kuu ya Tanzania iliendelea kutoa kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia benki na taasisi za fedha ili kuhakikisha sekta ya benki inabaki kuwa thabiti, imara na himilivu.

Katika kipindi hicho, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa kanuni mbalimbali ikiwemo kanuni za usimamizi wa biashara ya fedha za kigeni, kanuni za kutoa leseni ya benki na taasisi za fedha.

Pia,kanuni za utawala bora wa benki na taasisi za fedha, kanuni za usimamizi wa benki za maendeleo,kanuni za mitaji ya benki na taasisi za fedha.

Ikiwemo kanuni za ukwasi wa benki na taasisi za fedha, kanuni za kuchukua hatua stahiki kwa benki na taasisi za fedha na kanuni za usimamizi wa mikopo ya karadha kwa benki na taasisi za fedha.

"Aidha, Benki Kuu ilitoa miongozo ya matumizi ya fedha za kigeni katika kufanya malipo ndani ya nchi pamoja na utekelezaji wa makubaliano ya pili na tatu kuhusu usimamizi wa benki na taasisi za fedha (Basel II na III)."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news