Sekta ya Fedha yaendelea kuimarika huku vihatarishi vikipungua nchini

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Fedha imesema,sekta ya fedha nchini imeendelea kuwa imara huku vihatarishi vikipungua kutokana na matarajio ya uchumi wa Dunia kuendelea kuimarika.
Hayo yamesemwa leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

Aidha, amesema kwa mwaka 2023/24, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilipanga kukuza wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) kwa kiwango kisichopungua asilimia 10 ili kuendana na mahitaji ya shughuli za kiuchumi.

Pia,kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, kudhibiti na kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Waziri Dkt.Nchemba amesema, kutokana na mabadiliko ya mifumo ya usimamizi wa uchumi, Benki Kuu ya Tanzania ilianza kutumia mfumo mpya unaotumia riba ya benki kuu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sera ya fedha, usimamizi wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla.

"Utaratibu wa kutumia Riba ya Benki Kuu katika utekelezaji wa sera ya fedha, sekta ya fedha na uchumi jumla unaenda sambamba na mabadiliko ya mfumo wa utoaji taarifa kwa umma.

"Mheshimiwa Spika, licha ya kukabiliwa na changamoto ya mwenendo usioridhisha wa uchumi wa dunia, ukwasi katika uchumi ulitosheleza mahitaji ya shughuli za uzalishaji ambapo ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi - M3 ulikua kwa wastani wa asilimia 15.5 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2023/24, ikilinganishwa na lengo la asilimia 10.1."

Aidha, amesema mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kufikia ukuaji wa wastani wa asilimia 19.2 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023/24 ikilinganishwa na malengo ya ukuaji wa asilimia 16.4.

Vilevile, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.5 Desemba 2023 ikilinganishwa na dola bilioni 5.4 Juni 2023, kiwango kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.5, ikiwa ndani ya lengo la nchi la wastani wa miezi 4. 51.

"Mheshimiwa Spika, sekta ya fedha imeendelea kuwa imara, na vihatarishi kupungua kutokana na matarajio ya uchumi wa dunia kuendelea kuimarika.

"Sekta ya kibenki ambayo ni sehemu kubwa ya sekta ya fedha imeendelea kuwa imara, yenye kutengeneza faida, ukwasi na mtaji wa kutosha."

Waziri Dkt.Nchemba amesema, ubora wa rasilimali uliendelea kuongezeka, ambapo uwiano wa mikopo chechefu ulipungua hadi asilimia 4.3 Desemba 2023 kutoka asilimia 5.5 Juni 2023.

Amesema, hali hiyo inaashiria kuendelea kupungua kwa vihatarishi katika utoaji wa mikopo kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi.

Sambamba na hatua za kisera na kiusimamizi zinazoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania ili kupunguza mikopo chechefu.

"Utekelezaji wa sera ya fedha katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 umewezesha riba ya mikopo ya siku saba katika soko la jumla la fedha baina ya benki kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3.5 hadi 7.5.

"Wastani wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulifikia asilimia 17 ambapo sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa kwenye shughuli za kilimo, uchimbaji wa madini, usafirishaji na uzalishaji viwandani."

Waziri Dkt.Nchemba amesema, sekta ndogo ya benki imeendelea kuwa na ukwasi na mtaji wa kutosha, huku ikiendelea kutengeneza faida na uwiano wa mikopo chechefu kuendelea kuwa chini ya asilimia 5 ya mikopo yote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news