Serikali kuongeza uzalishaji wa mbegu za miti ya asili nchini

NA HAPPINESS SHAYO

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa, katika kuhakikisha kunakuwapo na vyanzo endelevu vya uzalishaji wa mbegu bora za miti sambamba na ulimaji miti hiyo kibiashara, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeanzisha upandaji wa miti jamii ya Mninga.

Ni katika mashamba yake ya Miti ya Ruvu lililoko Kibaha – Pwani, Mpepo lililoko Nyasa – Ruvuma na Shamba la Mbegu za miti Kising’a lililoko Mkoa wa Iringa.
Ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Mhe. Joseph George Kakunda aliyetaka kujua lini Serikali itazalisha mbegu za Mti wa Mninga ili kufanya mti huo kuwa zao la kibiashara.

Ameongeza kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imefanikiwa kuzalisha na kugawa kwa wadau mbalimbali jumla ya miche ya mninga 5,115 kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024.

’’Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TFS ilikusanya jumla ya kilo 237 za mbegu za Mninga kutoka katika vyanzo mbalimbali na ilifanikiwa kuzalisha na kugawa kwa wadau mbalimbali jumla ya miche ya mninga 5,115.”

Amesema pamoja na jitihada hizo, Serikali imejizatiti kuongeza ukusanyaji wa mbegu, kuotesha na kusambaza mbegu bora na miche ya Mninga kwa wadau mbalimbali kupitia vituo vyake vya uzalishaji mbegu za miti. Aidha, amesema Serikali itaendelea kuhamasisha taasisi za sekta binafsi pamoja na muungano wa wananchi kupitia vyama mbalimbali vya wakulima wa miti ili waweze kupanda miti hiyo ambayo inaweza kuwa adimu na kutoweka badala ya kupoteza fedha kuagiza mbegu za miche kutoka nchi za jirani kama Zimbabwe.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki ameweka bayana kuwa Tanzania imekuwa ikipokea wageni kutoka nchi za jirani wakija kujifunza kuhusu upandaji miti na hivyo Serikali itajitosheleza katika mbegu hizo za miti bora ambayo imeanza kupotea kwa mahitaji ya ndani na kuuza nje ili kupata fedha za kigeni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news