Serikali Kuu yapokea gawio la shilingi bilioni 27.4 kutoka Benki ya CRDB

NA PETER HAULE
WF

WAZIRI wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Serikali imepokea gawio la kiasi cha shilingi bilioni 27.4 kutoka Benki ya CRDB kutokana na Serikali Kuu kumiliki asilimia 21 ya Benki hiyo kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja na Serikali ya Denmark (DIF).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akimkabidhi Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justin, gawio kwa niaba ya Serikali Kuu la Shilingi Bilioni 27.4 kutoka Benki ya CRDB liliyotolewa kwenye faida mwaka 2023, jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati wa hafla ya Benki ya CRDB kuikabidhi gawio la mwaka 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, akiishukuru Benki ya CRDB kwa kutoa gawio la Shilingi Bilioni 27.4 kwa Serikali Kuu inayomiliki asilimia 21 za Benki hiyo, hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

Prof. Mkumbo alisema kuwa gawio hilo litatumika kuwaletea maendeleo wananchi hasa katika kuimarisha sekta ya afya kwenye eneo la miundombinu na kusaidia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

”Nimefurahi pia kuona taasisi na mashirika ya Serikali na Halmashauri pia wanapokea gawio la jumla ya shilingi bilioni 24.32, hivyo, jumla kuu ya gawio tunalolipokea leo ni shilingi bilioni 51.72,”alisema Prof. Mkumbo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akiukabidhi Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar gawio la shilingi milioni 752.4 kutoka Benki ya CRDB liliyotolewa kwenye faida ya mwaka 2023, jijini Dodoma.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza vituo vya afya kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 9,693 mwaka 2024, ikiwa ni pamoja na zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, rufaa, kanda na zile za Taifa.
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justin, akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kuhusu umuhimu wa taasisi kutoa gawio kwa maendeleo ya nchi baada ya kupokea gawio la Serikali Kuu la kiasi cha shilingi Bilioni 27.4 kutoka Benki ya CRDB liliyotolewa kwenye faida mwaka 2023, jijini Dodoma.

Alisema ongezeko hilo pia limekwenda sambamba na kuongezwa kwa vifaatiba vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa ikiwemo MRI kutoka 7 hadi 13, CT-Scan kutoka 12 hadi 45, Digital X-RAY kutoka 147 hadi 346, Ultrasound kutoka 476 hadi 668, Echocardiogram kutoka 95 hadi 102, Cathlab kutoka 1 hadi 4, na kununua Pet Scan 1 inayotumika kutolea huduma kwenye matibabu ya saratani.

Prof. Mkumbo amewapongeza viongozi wa Benki ya CRDB kwa utendaji mahiri ulioiwezesha Benki kuendelea kupata faida na kutoa gawio kwa Serikali na wanahisa wengine, kuwa vinara katika kulipa kodi, na kuongeza huduma jumuishi za fedha ikiwa ni pamoja na kutoa huduma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, akieleza maadhimio ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Benki hiyo ambapo walipitisha azimio la gawio la shilingi 50 kwa kila hisa ambalo ni ongezeko la asilimia 11 kwa mwaka 2023, ikilinganishwa na gawio la shilingi 45 kwa mwaka 2022, jijini Dodoma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alisema kuwa kutokana na matokeo mazuri ya kifedha iliyopata Benki kwa mwaka 2023, wanahisa wa Benki hiyo katika Mkutano Mkuu walipitisha azimio la gawio la shilingi 50 kwa kila hisa ambalo ni ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na gawio la shilingi 45 kwa mwaka 2022.
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) (katikati), wakiwa katika hafla ya Benki ya CRDB kukabidhi gawio la mwaka 2023 kwa Serikali, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), jijini Dodoma.

Alisema kuwa jambo hilo linaonesha ukuaji endelevu wa uwekezaji wa wanahisa ndani ya Benki hiyo ambapo jumla ya gawio lote lililotolewa mwaka huu ni shilingi bilioni 130.6 sawa na asilimia 31.8 ya faida halisi iliyopatika.
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) (katikati), ikiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Fedha baada ya hafla ya Benki ya CRDB kukabidhi gawio la mwaka 2023 kwa Serikali, jijini Dodoma. Mhe. Prof. Mkumbo, alimwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Kameck Nchemba Madelu (Mb) kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hilo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Olan Manase Njenza (Mb), alisema kuwa kazi kubwa imefanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya Benki na gawio hilo ni matunda ya uwekezaji wa muda mrefu wa Serikali.
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) (katikati), ikiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Benki ya CRDB, baada ya hafla ya Benki ya CRDB kukabidhi gawio la mwaka 2023 kwa Serikali, jijini Dodoma. Mhe. Prof. Mkumbo, alimwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Kameck Nchemba Madelu (Mb) kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hilo.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -Wizara ya Fedha).

Ameziomba Benki kuangalia namna bora ya kuwekeza ili kuboresha uchumi wa Tanzania katika sekta za Kilimo, madini, utalii na sekta nyingine za uzalishaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news