NA ANGELA MSIMBIRA
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Zainab Katimba amemuagiza Mkandarasi M/s CRJE East Africa LTD kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara Wafipa - Kagera na Bangwe- Burega kwa wakati.
Mhe. Katimba ametoa kauli hiyo Mei 31, 2024 wakati alipokagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Bongwe, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.
Amemtaka, Mkandarasi kufuata sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa kwenye mikataba ambayo inaeleza wazi barabara hiyo inatakiwa kukamilika lini ili wananchi waweze kupata huduma za usafirishaji.
"Wakandarasi mnapopatiwa kazi jukumu lenu ni kutekeleza kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa kwa kuwa mnapokuwa nyuma ya ratiba mnakwamisha maendeleo ya wananchi."
Amemtaka kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati kwa kuwa wananchi wanamatarajio makubwa na Serikali inahitaji kuona fedha inayotengwa kwa ajili ya ujenzi inaleta matokeo chanya.
Aidha, amesema Serikali haitafumbia macho ucheleweshaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara ama kusuasua kwa utekelezaji wa miradi nchini.
Naye Diwani wa Kata ya Bangwe, Mhe. Hamis Besere amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Kigoma.