Serikali yatoa shilingi bilioni 49.78 kwa wajasiriamali wadogo kupitia Self Microfinance Fund

NA GODFREY NNKO

ZAIDI ya wajasiriamali wadogo 37,024 wamenufaika kupitia mikopo yenye masharti nafuu ya thamani ya shilingi bilioni 49.78 kutoka Mfuko wa Huduma Ndogo za Fedha (SELF Microfinance Fund) ndani ya mwaka 2023.
Hayo yamesemwa leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

Amesema, katika mwaka 2023 mfuko huo ulipanga kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya shilingi bilioni 44.8 kwa wajasiriamali 38,000.

Vile vile,urejeshaji wa mikopo usipungue asilimia 95 na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa walengwa au wanufaika 5,500 nchini.

"Hadi Desemba 2023, mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 49.78, sawa na ufanisi wa asilimia 111 ya lengo kwa wajasiriamali wadogo 37,024, sawa na ufanisi wa asilimia 97 ya lengo la mwaka.

"Aidha, kiwango cha urejeshaji wa mikopo kilifikia asilimia 95.87 dhidi ya lengo la asilimia 95 kwa mwaka 2023.

"Vilevile, mfuko umetoa elimu kwa wadau 2,705, sawa na asilimia 49.1 ya lengo la mwaka. Sababu ya kutofikia lengo la elimu ni kutokana na mfuko kusitisha utoaji wa mikopo ya vikundi ili kufanya mapitio ya mfumo wa usimamizi wa mikopo kwa vikundi."

Mfuko wa SELF (SELF Microfinance Fund) ambao upo chini ya Wizara ya Fedha ni zao la Mradi wa Serikali ambao ulijulikana kama Small Entrepreneurs Loan Facility (SELF) ulioanzishwa mwaka 1999.

SELF Project ilikuwa ni miongoni mwa programu za Serikali zinazotekeleza jukumu la kupunguza umaskini kwa niaba ya Serikali ambayo ilifadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).

Mradi ulilenga katika kuongeza mchango wa biashara ndogo za kati katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kuimarisha tasnia ya mikopo midogo midogo nchini Tanzania.

Aidha, mfuko huu wa kifeha una jukumu la kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wenye kipato cha chini nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news