DAR- Aliyekuwa Mtendaji wa Mtaa wa Oysterbay katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Chema Hamis Kalembo amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela bila faini, kwa ubadhirifu wa shilingi milioni 12 za makusanyo ya ada ya taka mtaani.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 24, 2024 kupitia kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 11/2022 mbele ya Mheshimiwa Isiaqa Kuppa, Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Katika shauri hilo lililoendeshwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Janeth Kafuko, Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo kwa kosa la ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 RE 2019].
Vikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu uchumi Paragraph 21 ya Jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Ifahamike kuwa, mshtakiwa akiwa Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay alitenda kosa hilo la ubadhirifu wa fedha za umma kiasi cha shilingi 12,000,000.
Fedha ambazo zilikuwa ni za makusanyo ya ada ya taka alizotakiwa kuziwasilisha benki na badala yake kuzitumia kwa matumizi yake biafsi.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka yoyote.
Tags
Habari
Mahakama
Mahakamani Leo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania