STAMICO yaeleza mipango kabambe ya uwekezaji kwa Kamati ya Bunge

DODOMA-Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupitia kampuni tanzu ya STAMIGOLD leo Juni 11, 2024 limewasilisha mpango wa uwekezaji wa kampuni ya STAMIGOLD kuhusu uendelezaji wa miradi ya madini kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo,Deusdedith Magala amesema kuwa tangu kuanza uzalishaji hadi kufikia Machi, 2024 mgodi umezalisha na kuuza jumla ya wakia 122,964.53 za madini ya dhahabu na wakia 16,662.54 ya madini ya fedha.
Magala ameeleza kuwa mgodi umeendelea na uhakiki na utafiti kupitia njia mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa na ukadiriaji upya wa akiba ya mashapo ya mgodi ambapo mpaka April, 2024 mgodi ulikuwa na akiba ya mashapo ya wakia za dhahabu 114,190 ambazo zitachimbwa kwa miaka mitano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Nishati na Madini, Mathayo David Mathayo ameitaka wizara kuisimamia na kufuatilia kwa karibu kampuni ya STAMIGOLD ili iwe kampuni yenye manufaa.

Akizungumza kuhusu wajibu wa mgodi kwa jamii (CSR),Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amesema kuwa wizara imepokea maoni yaliyowasilishwa na kamati kuhusu mapitio ya kanuni za CSR na kuzifanyia kazi ya kuziboresha itakapobidi.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Madini,Kheri Mahimbali amesema Malengo ya Wizara ni kuipeleka mbali Stamigold ili uwe mgodi mkubwa utakaotambaa sehemu mbalimbali ndani ya nchi pamoja na kutambulika na taasisi kubwa za fedha.
STAMICO ilianzishwa rasmi mwaka 1972 kwa lengo la kuwekeza kimkakati katika miradi ya madini na uvunaji wa rasilimali madini ndani ya mnyororo mzima wa sekta ya madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news