STAMICO,KOMIR ya Korea waingia makubaliano kuendeleza madini ya kimkakati nchini

SEOUL-Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo Juni 4, 2024 limesaini hati ya makubaliano (MoU) na Shirika la Ukarabati wa Migodi na Rasilimali za Madini la nchini Korea (KOMIR) ili kuendeleza rasilimali madini ya kimkakati nchini pamoja na kubadilishana uzoefu.
Hati hiyo imesainiwa jijini Seoul nchini Korea kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse na Rais ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa KOMIR Bw. Hwang, Kyu-Yearn na kusimamiwa na Waziri wa Biashara,Viwanda na Nishati wa Korea Kusini Bw.Inkyo Cheong.
Makubaliano hayo ni ya miaka mitatu na hati hiyo itahusisha ushirikiano kwenye uendelezaji wa madini ya kimkakati na kubadilishana uzoefu.

Makubaliano hayo ni matunda ya uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili pamoja na ziara rasmi ya kikazi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan nchi ya Jamhuri ya Korea iliyoanza rasmi tarehe 2 June 2024 na kutarajiwa kuhitimishwa tarehe 6 Juni 2024.

Katika hafla hiyo, Dkt. Mwasse amesema Tanzania na Korea zimelenga kushirikiana katika masuala ya utafiti, uwekezaji, uchimbaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati yanayopatikana nchini Tanzania.
Ikumbukwe STAMICO ni miongoni mwa Taasisi zilizoshiriki katika ziara rasmi ya kikazi ya Mhe. Rais nchini Korea ya Kusini na kupitia utiaji sahihi wa hati hii utaongeza chachu katika masuala ya tafiti za Madini ya kimkakati kama vile graphite lithium, nikel cobalt, manganese pamoja na uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya Madini kwa ujumla kati ya nchi hizo mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news