Taasisi za uwekezaji nchini zatakiwa kujitangaza

NA JOSEPHINE MAJULA

TAASISI za Uwekezaji nchini zimetakiwa kuongeza wigo wa kujitangaza na kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma wanazotoa ili kuongeza Wawekezaji na kuiongezea Serikali mapato.
Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella John, akiwaonesha baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, kalenda ya Mpango wa Uwekezaji ya Mwaka baada ya kumalizika kwa semina ya elimu ya fedha kwa watumishi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano mkoani hapo.

Ushauri huo umetolewa na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, baada ya kumalizika kwa semina ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata elimu hiyo, Afisa Kilimo wa Mkoa wa Tabora Bi. Eunice John, alisema kuwa Watumishi ni wengi ila hawana elimu ya uwekezaji, bidhaa zinazopatikana katika Taasisi za Uwekezaji na vihatarishi vilivyopo ili wafanye maamuzi sahihi katika kuwekeza.
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, akieleza umuhimu wa kuweka akiba kwa Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, wakati wa semina ya elimu ya fedha kwa Watumishi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano mkoani hapo.

“Binafsi sijawahi kupata elimu kutoka taasisi ya Uwekezaji yoyote hapa nchini zaidi ya kusikia kwa watu, kuna fursa nzuri katika taasisi hizo zenye faida kubwa ukiwekeza mtaji mkubwa,” alisema Bi. Eunice John.

Alisema kuwa kila mtumishi anahitaji sana elimu katika masuala ya uwekezaji ili aweze kufanya maamuzi ya kuwekeza ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi, na kwamba bila kupata elimu ya huduma zinazotolewa na kujua upatikanaji wa faida hakuna mwananchi ataweka fedha zake kwenye taasisi hizo.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, wakifuatilia mada mbalimbali kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Tabora.

Naye Mtumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Martin Peter, alisema kupitia elimu ya fedha aliyoipata ataanza kujiwekea akiba na atajiepusha ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo hayamuongezei kipato.

“Nitaendelea kuwa Balozi kwa Watumishi wenzangu ili elimu niliyoipata ikawanufaishe nao na kuwashawishi kujijengea utamaduni wa kujiwekea akiba na kufanya uwekezaji ili watakapo staafu wasitetereke kiuchumi na kupata magonjwa ambayo yanatokana na mawazo ya kukosa fedha ya kukidhi mahitaji,” alisema Bw. Martin Peter.

Naye Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella John, aliwapongeza watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha.

“Mwitikio umekua mkubwa sana kwa Watumishi hawa, naamini elimu tuliyowapatia wameielewa vizuri hali iliyosababisha watumishi wengi kuonesha nia ya kufungua akaunti na kuahidi kufanya uwekezaji, lakini pia kuna watumishi wengine tumewafungulia akaunti hapa hapa za mifuko mbalimbali kwa ajili ya kufanya uwekezaji, alisema Bi. Stella John.
Afisa Maendeleo Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Panin Kerika akifafanua jambo wakati wa semina kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Tabora.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Tabora).

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Tabora katika Wilaya nne ya Sikonge, Urambo, Uyui na Tabora Manispaa, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news