TAKUKURU mguu sawa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, yawakutanisha viongozi wa asasi za kiraia

DAR-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana ma Rushwa Tanzania (TAKUKURU) imekutana na viongozi wa Asasi za Kiraia na Asasi zisizo za kiserikali kwa lengo la kujadili na kuweka mkakati wa kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Akizungumza katika warsha ya siku moja iliyowakutanisha viongozi hao leo Juni 26,2024 jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo,CP Salum Rashid Hamduni amesema,

"Kama mnavyofahamu mwaka huu wa 2024, tutakuwa na Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa na mwakani, 2025 tutakuwa na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

"Vitendo vya rushwa katika uchaguzi vinasababisha kuwa na uchaguzi usiozingatia misingi ya haki na usawa na hili limekuwa ni tatizo la kidunia ambapo hata Tanzania haijaachwa salama."

Amesema, tatizo hilo limeifanya TAKUKURU kuendelea kubuni mikakati ya kuikabili rushwa katika uchaguzi kwa kuwa madhara yake ni makubwa sana.

Pia,TAKUKURU inatambua mchango wao mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa ndio sababu ikaandaa warsha hiyo ili kwa pamoja washirikiane kukabiliana na tatizo hilo la rushwa katika chaguzi nchini.

Amesema,rushwa katika uchaguzi ina madhara mengi sana, ikiwa ni pamoja na upatikanaji viongozi wasio waadilifu, wanaojihusisha na vitendo ya rushwa pamoja na kutozingatia misingi ya haki.

Vilevile kukosekana usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo mambo ambayo ni ya muhimu katika ustawi wa wananchi.

"Udhoofisha utawala bora na demokrasia, ambapo baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora hushindwa kugombea au kutoteuliwa na kutochaguliwa kwa kutokuwa kuwa tayari kutoa hongo."

CP Hamduni amesema, rushwa pia husababisha uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa na kusababisha Taifa kuendelea kughubikwa na rushwa.

Jambo lingine amesema, rushwa huwa inasababisha wananchi kukosa imani na Serikali na hata kusababisha machafuko.

"Na la kusikitisha zaidi ni kudhalilisha utu kwa kufananisha thamani ya mtu na hongo (feďha, nguo, chakula anayopewa ili apige au asipige kura).

Amesema, kutokana ukubwa wa athari zinazoweza kusababishwa na vitendo ya rushwa katika uchaguzi, TAKUKURU imeona ni busara kukutana na viongozi wa asasi za kiraia, kwa lengo la kujadili tatizo la rushwa katika uchaguzi,

Madhara yake na kisha kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kupambana nayo kabla madhara hayajatokea, kwani TAKUKURU peke yake haiwezi kutekeleza jukumu hilo la kuzuia na kupambana na rushwa.

Amesema,anatambua kuwa asasi za kiraia zimekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na usawa, kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutambua haki na wajibu wao katika masuala mbalimbali ya kijami,kiuchumi na kisiasa ikiwemo kushiriki katika uchaguzi pamoja na shughuli za maendeleo.

Pia amesema,asasi za kiraia zimeendelea kusaidia Serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kwa kufuatilia utendaji wa Serikali, uwajibikaji wa watendaji wa Serikali pamoja na
kuhamasisha wananchi kushiriki mapambano dhidi ya rushwa.

"TAKUKURU inatambua na kuthamini sana mchango huu wa asasi za kiraia kwa jamii na Taifa kwa ujumla."

Amesema, vile vile anatambua kuwa utendaji kazi wao umewafanya wawe karibu zaidi na jamii jambo ambalo linawafanya kuwa na ufahamu mzuri wa changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo changamoto ya rushwa.

"Ukaribu huu walionao kwa jamii unawafanya kuwa kundi muhimu sana ambalo linaweza kusaidia kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi.

"TAKUKURU inaamini ushiriki wenu wa moja kwa moja katika kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo ya rushwa kwenye uchaguzi una faida kubwa kwa Taifa, jamii na mtu mmoja mmoja ambapo faida hizo ni pamoja na kuchaguliwa kwa viongozi bora watakaoongoza kwa mujibu wa sheria na kutekeleza mipango ya maendeleo."

Amesema, warsha hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikaliza kudhibiti rushwa katika uchaguzi ambazo serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezianza na inaendelea nazo ambapo mpaka sasa imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki na usioghubikwa na vitendo vya rushwa.

CP Hamduni ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchagazi (INEC),kutunga Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, 2024;kutunga kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024,kuendelea na maboresho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 na,

Kuiwezesha zaidi TAKUKURU ili kwa kushirikiana na wadau wengine, iweze kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi ambapo warsha hiyo ni sehemu ya uwezeshaji huo.

Amesema, pamoja na jitahada hizo za Serikali, TAKUKURU nayo haijabaki nyuma ambapo kwa kuzingatia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 imejizatiti kikamilifu kuendelea kutimiza wajibu wake wa kuzuia na kupambana rushwa hapa nchini ikiwemo katika uchaguzi kwa kufanya mambo kadhaa.

Miononi mwa mambo hayo ni kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi ili waweze kuchagua viongozi waadilifu.

"Na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha wananchi kutojihusisha na vitendo vya rushwa ikiwamo rushwa katika uchaguzi.

"Warsha hii ni sehemu ya utekelezaji huu na bado tutakutana na makundi mengine ya wadau ili kujipanga kwa pamoja,kufanya kazi za utafiti na udhibiti kwa lengo la kubainisha mianya ya rushwa katika uchaguzi na kushauri namna bora ya kuiziba.

"Pia, kuchukua hatua za haraka kuzuia vitendo vya rushwa na kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kufanya uchunguzi na kuendesha mashtaka.

"Dhamira hii nzuri ya Serikali haiwezi kufanikiwa pasipo ushiriki wa wananchi pamoja na wadau mbalimbali mkiwemo Asasi za Kiraia, ndiyo sababu ya uwepo wa warsha hii."

CP Hamduni amewataka washiriki kutumia fursa hiyo muhimu ya kuijenga Tanzania ambayo viongozi wake wanapatikana bila kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news