TAKUKURU yasema Uchaguzi bila rushwa inawezekana

DAR-Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU),CP Salum Rashid Hamduni amesema kuwa, utekelezaji wa mpango mkakati wa kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 utatekelezwa baada ya kumaliza kukusanya na kuyachakata maoni yaliyotolewa na wadau.
CP Hamduni amebainisha hayo leo Juni 28,2024 jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua warsha ya siku moja iliyowakutanisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Ni kwa lengo la kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025. 

Pia, amesisitiza kuwa, chaguzi zote kuanzia wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu bila rushwa inawezekana kwa ustawi bora wa Taifa kupitia viongozi watakaochaguliwa,

Amesema kuwa, suala hilo ni mtambuka na kwamba Uchaguzi unawahusu wadau wengi wakiwemo TAKUKURU, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),wagombea na vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea na ndio maana wameanza kukutana na wadau tofauti tofauti.

"Yale yanayotuhusu kama taasisi tutayawekea utaratibu wa utekelezaji na yale yanayohusu taasisi zingine tutatoa ushauri kwa kuwa moja ya majukumu ya taasisi hii ni kushauri."

Akifungua warsha hiyo Hamduni amesema, "kama mnavyofahamu mwaka huu 2024, tutakuwa na Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa na mwakani, 2025, tutakuwa na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Vitendo vya rushwa katika uchaguzi vinasababisha kuwa na uchaguzi usiozingatia misingi ya haki na usawa.na hili limekuwa ni tatizo la kidunia ambapo hata Tanzania haijaachwa salama."

Amesema, tatizo hilo limeifanya TAKUKURU kuendelea kubuni mikakati ya kuikabili rushwa katika uchaguzi kwa kuwa madhara yake ni makubwa sana.
Pia, amesema TAKUKURU inatambua mchango mkubwa wa wadau wa habari katika mapambano dhidi ya rushwa ndio sababu ikaandaa warsha hiyo ili kushirikiana kukabiliana na tatizo hilo la rushwa katika chaguzi nchini.

Ametaja baadhi ya madhara ya rushwa katika uchaguzi kuwa ni pamoja na upatikanaji viongozi wasio waadilifu, wanaojhusisha na vitendo ya rushwa pamoja na kutozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo.


CP Hamduni amesema, hayo ni mambo ambayo ni ya muhimu katika ustawi wa wananchi.

Pia, amesema udhoofisha utawala bora na demokrasia, ambapo baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora hushindwa kugombea au kutoteuliwa ama kutochaguliwa kwa kutokuwa kuwa tayari kutoa hongo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wahariri,Mgaya Kingoba kutoka Gazeti la Habarileo ameishukuru taasisi hiyo kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwashirikisha kutoa maoni yao.
Amesema, vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuisaidia TAKUKURU kupitia kalamu zao na kuwataka waandishi wa habari kutumia nafasi zao kwa kubainisha kwa jamii madhara ya rushwa na namna ya kukomesha vitendo hivyo.

Aidha,ameiomba TAKUKURU kuendelea kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari ili kuweza kukomesha vitendo vya rushwa kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania na watanzania kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news