Tanga tujitokeze kwa wingi kesho kumpokea Katibu Mkuu Balozi Dkt.Nchimbi-Selemani Sankwa

TANGA-Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Selemani Sankwa ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Tanga kujitokeza kwa wingi kupokea ugeni wa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye ataingia mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia Juni 7 hadi 8, 2024 huku akiongozana na viongozi wengine wa chama.
Sankwa amesema hayo leo Juni 6, 2024 ofisini kwake wakati akiongea na waandishi wa habari. 

Kuhusu ziara hiyo ya Mtendaji Mkuu wa Chama Taifa, amesema ujio wake mkoani humo umelenga kuimarisha uhai wa chama, kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi. 

“Niwaombe wakazi wa Tanga na wilaya zake zote, kujitokeza kwa wingi kesho kuwapokea viongozi wetu wa Chama Taifa wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama Taifa Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi. 

"Ujio wa viongozi hawa una manufaa makubwa kwani kupitia wao watasaidia kusukuma baadhi ya miradi ambayo imekwama ili iweze kutekelezwa kikamilifu” amesema Sankwa.

Katika hatua nyingine, Sankwa amesema ziara hiyo itasaidia kuimarisha zaidi na kuendeleza umoja wa WanaCCM wa mkoa wa Tanga. 

Pia, amesema ni muhimu kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwani ni kawaida kwa viongozi hao kutoa fursa kwa wananchi kueleza kero zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa ustawi wao.

Pamoja na hayo, Sankwa amesema kwa kuwa CCM imeomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi, ni lazima kero za wananchi zipatiwe ufumbuzi kwani hiyo ndiyo ajenda kuu ya CCM ya kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa wakati.

Sankwa ametoa ratiba ya ziara ya viongozi hao huku ikionesha kuanzia Juni 7, viongozi hao watakuwa na mkutano wa hadhara katika uwanja vya Stendi ya Mombo kuanzia saa 5 Asubuhi. Baadaye saa 7 Mchana wanatarajiwa kufanya mkutano mwingine Korogwe katika uwanja wa soko la zamani. 

Juni 8 watahitimisha ziara yao Jijini Tanga ambapo watafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Lamore kuanzia saa 8 mchana. 

Aidha, Katibu Mkuu Balozi Dk. Nchimbi pamoja na timu yake wanatarajiwa kufanya mkutano wa ndani pamoja na kuzindua kiwanda cha Tanga Cable kilichopo karibu na uwanja wa Ndege Tanga Mjini.

Katika ziara hiyo, Dk. Nchimbi anatarajiwa kuongozana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA Amos Gabriel Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Hamid Abdallah. Viongozi hawa wataingia mkoani Tanga wakitokea Kilimanjaro kwa ziara ya kujenga chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news