Tanzania, Guinea Bissau zakubaliana mambo haya

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Guinea-Bissau zimekubaliana kukuza ushirikiano na uhusiano katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema hayo leo Juni 22,2024 wakati yeye na mgeni wake Rais wa Jamhri ya Guinea-Bissau Mhe. Umaro Sissoco Embaló walipokuwa wakizungumza na vyombo vya habari katika hafla iliyofanyika Ikulu wakati wa ziara ya Rais huyo.

Awali katika mazungumzo yao, marais hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kuendeleza uzalishaji wa zao la korosho hasa kupitia tafiti ili kuweza kuimarisha mnyonyoro mzima wa thamani wa zao hilo.

Sambamba na kuanzisha vyama vya ushirikiano ili kukuza zao na bei ya zao hilo katika Soko la Dunia.

Masuala mengine waliojadiliana ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji ikiwemo kuimarisha ushirikiano kwenye sekta za uchumi wa buluu, sekta za afya, elimu, ulinzi na usalama pamoja na masuala ya kimataifa.

Rais Dkt.Samia pia amesema ziara ya Rais Embaló imefungua upya milango ya ushirikiano na mahusiano.

Ameyasema hayo baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa mwongozo wa ushirikiano ambao utaimarisha zaidi ushirikiano uliopo kwa manufaa ya nchi hizo mbili na wananchi wake. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ziara ya Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Guinea-Bissau Mhe. Umaro Sissoco Embaló Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 22 Juni, 2024.

Kwa upande wake Rais Embaló ametambua na kushukuru mchango wa Tanzania kwenye ukombozi wa bara la Afrika ikiwemo Guinea-Bissau.

Rais huyo pia alitumia fursa hiyo kumualika Rais Samia kufanya ziara nchini humo. Aidha, Rais Embaló amewakaribisha wadau wa sekta binafsi nchini kutumia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) kuwekeza nchini Guinea-Bissau na kutumia nchi hiyo kama lango la kukuza biashara na ukanda wa Afrika Magharibi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news