Tanzania kinara Afrika kimahakama katika matumizi sahihi ya fedha za Benki ya Dunia,TEHAMA

WASHINGTON DC-Tanzania imeonekana kuwa kinara Barani Afrika katika masuala ya matumizi mazuri na sahihi ya fedha za Benki ya Dunia na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Bi. Christina Awor, Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Ukanda wa Afrika ya Mashariki (kushoto),Mhe. Valentine A. Katema, Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar (kulia), na Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania wakati akisisitiza jambo katika Mkutano wa Benki ya Dunia tarehe 25 Juni, 2024 Jijini Washinton DC, Marekani.

Hilo limebainika katika Mkutano wa siku mbili unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Benki ya Dunia (WB) jijini Washngton nchini Marekani ambapo Washiriki wa Mkutano huo ni Wajumbe kutoka nchi mbalimbali duniani ambazo zimepewa mikopo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia utoaji wa haki huku Tanzania ikiwakilishwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.

Akizungumza kutoka jijini Washngton, Prof. Ole Gabriel alisema kwa msingi huo na baada ya Tanzania kuibuka kinara, viongozi wa Benki ya Dunia wamefurahishwa na kufarijika sana kwani pamoja na matokeo chanya hayo nchi kadhaa Barani Afrika ikiwemo Liberia, Ghana na nyinginezo zimeonesha nia ya dhati kuja kujifunza zaidi nchini Tanzania ili kuweza kubaini siri na mbinu za mafanikio hayo.
Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (katikati), Bi. Christina Awor, Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Ukanda wa Afrika ya Mashariki (kulia) na Mhe. Valentine A. Katema, Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar (kushoto), katika picha ya pamoja baada ya Tanzania kuibuka kinara katika Mkutano wa Benki ya Dunia tarehe 25 Juni, 2024 Jijini Washinton DC, Marekani.

”Mambo makubwa matatu ambayo yamejiri hapa Mkutanoni, moja ni pamoja na nchi mbalimbali kuonyesha namna ambavyo wamefanikiwa katika masuala ya utoaji haki kwa Wananchi na Jamii yake kule wanakotoka na kutoa huduma za Kimahakama. Pili, kuweka Mipango Mkakati kwa ajili ya kuendeleza utoaji wa haki katika nchi mbalimbali na tatu ni jinsi gani ambavyo nchi zile ambazo zimefanikiwa kupata mikopo hiyo wataendeleza miradi hiyo baada ya Benki ya Dunia kumaliza muda wake wa ufadhili.” 

Pamoja na mambo hayo yaliyojiri Mkutanoni hapo, Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama alielezea namna ambavyo Mataifa mengine yamestaajabishwa na namna Tanzania imefanikiwa kupiga hatua katika maboresho ya huduma za Mahakama na kubainisha siri za mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya Viongozi Wakuu wa Mahakama ya Tanzania yaani Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (kulia waliokaa) na Mhe. Valentine A. Katema, Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar (kushoto waliokaa), katika tete-a-tete na Wajumbe wengine wa Mkutano huo (hawapo pichani) katika Mkutano wa Benki ya Dunia tarehe 25 Juni, 2024 Jijini Washinton DC, Marekani.

Prof. Ole Gabriel aliitaja siri ya pili ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Mhimili wa Mahakama ya Tanzania na Mhimili wa Serikali ambao ndio wenye mamlaka ya kukopa fedha na kulipa mikopo muhimu kwa Maendeleo Endelevu ya Taifa kwani Mahakama kwa asili ya huduma zake haifanyi biashara kuiwezesha kukopa na kulipa mikopo.

Vilevile aliitaja siri ya tatu ya mafanikio hayo ya maboresho ya huduma za Mahakama ya Tanzania kuwa ni pamoja na kuruhusu ugunduzi na uvumbuzi (Innovative Space) kwa Watumishi wa Mahakama ya Tanzania ili kuwapa nafasi wao pia kuwa sehemu ya wadadisi na kuongeza weledi wa kuweza kuchambua Mifumo ya TEHAMA na kuleta mageuzi makubwa yanayochagizwa zaidi na utendaji mzuri wa Majaji, Mahakimu na Watendaji wengine wa Mahakama ambao sio Mahakimu katika kutoa haki kwa Wananchi.
Mtendaji Mkuu huyo aliongeza kwa kusema kuwa Benki ya Dunia na Wajumbe wa Mkutano huo wamefurahishwa na kuridhishwa sana na namna ambavyo Mahakama ya Tanzania inatumia wadau wengine kama REPOA na Taasisi nyingine katika kuleta mageuzi.

Aidha, alimshukuru Kiongozi wa Mhimili wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, pamoja na Viongozi wengine Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Eva Kiaki Nkya.

Sambamba na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama, Mhe. Dkt.Angelo Rumisha (J), kwa namna na jinsi ambavyo wamekua vinara katika kusukuma masuala yote ya maboresho ya miundombinu ya utoaji haki na njia za kisasa za utoaji huduma za Mahakama kwa Wananchi na Wadau wake.
Prof. Ole Gabriel alitoa wito kwa Watanzania kujivunia utulivu, amani, upendo na mshikamano uliopo nchini ikiwa ni pamoja na mahusiano mazuri katika utendaji kazi wa Mihimili Mitatu ya Taifa la Tanzania na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya Viongozi wa Mihimili hiyo mitatu; Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson Mwansasu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania.
Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (aliyevaa tai), Bi. Christina Awor, Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Ukanda wa Afrika ya Mashariki (wa tano kutoka kushoto)na Mhe. Valentine A. Katema, Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar (wa nne kutoka kulia), katika picha ya pamoja na Wajumbe kutoka Mataifa mengine waliohudhuria Mkutano wa Benki ya Dunia tarehe 25 Juni, 2024 Jijini Washinton DC, Marekani. 

Kadhalika, Prof. Ole Gabriel aliushukuru Ubalozi wa Tanzania Jijini Washington DC ukiongozwa na Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza, kwa mapokezi mazuri ya ujumbe kutoka Tanzania chini ya Afisa wa Ubalozi Wa Tanzania Bw. Saidi Nyenge, ambao pamoja naye ameambatana na Mhe. Valentine Andrew Katema, Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar na Bi. Tina Awor, Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Lengo la Mkutano huo ni kushirikishana uzoefu wa nchi mbalimbali kuhusu faida za Miradi ya Benki ya Dunia kwenye kuimarisha Mnyororo wa Utoaji Haki ambapo Tanzania ni Kinara kwa Nchi za Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news