NA GODFREY NNKO
SERIKALI imewataka wanahabari nchini kutambua kuwa, wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii ili kuweza kushiriki kikamilifu katika masuala yao na ya Kitaifa ikiwemo ushiriki katika maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga nchini.
Wito huo unakuja ikiwa zimebaki siku chache kabla ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kuzindua rasmi zoezi la maboresho hayo mkoani Kigoma. Zoezi hilo litafanyika Julai Mosi,2024.
Hayo yamebainishwa leo Juni 14,2024 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na Meneja wa Huduma za Utangazaji,Mhandisi Andrew Kisaka kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ni katika siku ya pili ya mkutano kati ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ikiwa ni katika hatua ya kutoa elimu kwa wadau kuelekea katika mchakato wa maboresho ya daftari hilo nchini.
"Vyombo vya habari vina ushawishi mkubwa katika jamii. Ukiona jamii ya sasa hivi wanachozungumza, wanachojadiliana asilimia kubwa kinatokana na ushawishi wa vyombo vya habari."
Amesema, katika kuelimisha wananchi, lazima weledi, maadili katika taaluma vizingatiwe ili kuhakikisha umma unajisikia faraja kushiriki katika maboresho hayo bila kusita.
"Vile vile tunaunganisha jamii katika masuala ya Kitaifa na kuchochea maendeleo katika jamii,"amesisitiza huku maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yakiongozwa na kauli mbiu ya 'Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uongozi Bora'.
Pia, amewataka wanahabari kutambua kuwa wao ni watoa huduma katika jamii. "Na huduma inayotolewa inatambulika kuwa ni haki ya msingi wa kiraia. Kwa hiyo, products tunayoitoa ni haki ya kila mtu."
Vile vile, amesema kuna umuhimu kwa kila chombo cha habari kuandaa kipindi,makala na habari mahususi kuhusu maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.
INEC
Juni 13, 2024 wakati akifungua mkutano wa tume na wanahabari hao, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele aliwataka wanahabari kutumia vyombo vya habari kuwahabarisha na kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Pia, alisisitiza juu ya umuhimu wa vyombo vya habari na nafasi yao katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.
Mkutano huo ambao ni mwendelezo wa vikao vya wadau vilivyoanza Juni 07, 2024 ulikuwa na lengo la kuwapa wadau hao wa uchaguzi taarifa mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya kuanza rasmi kwa zoezi la uboreshaji wa daftari.
“Tume inatarajia kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwenu, kwa kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu zoezi lililopo mbele yetu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
"Na kuwahamasisha wananchi wenye sifa ya kujiandikisha kuwa wapiga kura, wajitokeze kwa wingi kwa tarehe ambazo Tume imeziweka kwa kila kituo,”amesema Jaji Mwambegele.
Tags
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Habari
INEC Tanzania
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA
TCRA Tanzania
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi