TIRA yakamilisha uchambuzi wa mikataba 344 ya bima mtawanyo kwa kampuni 29

NA GODRREY NNKO

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imekamilisha uchambuzi wa mikataba 344 ya bima mtawanyo kwa kampuni 29 sawa na asilimia 90.6 ya lengo.
Hayo yamesemwa leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

Amesema, katika mwaka 2023/24, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ilipanga kufanya uchambuzi wa mikataba ya bima mtawanyo kwa kampuni 32.

Vile vile, kufanya ukaguzi wa kampuni za bima, kuandaa mwongozo wa bima za kilimo, kuhamasisha wadau wa bima kuandaa bidhaa za sekta ya kilimo na kupokea na kushughulikia malalamiko ya wateja wa bima kwa wakati.

Aidha, Waziri Dkt.Nchemba amesema,Shirika la Bima la Taifa lilipanga kukamilisha taratibu za kupata ithibati ya cheti cha ubora cha utoaji huduma kwa wateja (ISO 9001:2015).

Pia, kuongeza wateja wapya 116 wa bidhaa za taasisi na kubuni bidhaa tatu mpya zitakazokidhi mahitaji ya soko.

"Hadi Aprili 2024, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imekamilisha uchambuzi wa mikataba 344 ya bima mtawanyo kwa kampuni 29 sawa na asilimia 90.6 ya lengo."

Amesema, pia mamlaka hiyo imefanya ukaguzi kwa wadau wa bima 259, kuandaa Mwongozo wa Bima za Kilimo na kampuni 14 za bima zimeanzisha Konsotia ya Kilimo-Tanzania Agriculture Insurance Consortium (TAIC) iliyozinduliwa Julai 1, 2023.

Waziri Dkt.Nchemba amesema, mamlaka imepokea na kushughulikia malalamiko 288 ya wateja wa bima nchini.

"Vilevile, Shirika la Bima la Taifa limefanikiwa kupata ithibati ya cheti cha ubora cha ISO 9001:2015 pamoja na cheti cha ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania na kuandikisha wateja wapya 222 sawa na ufanisi wa asilimia 191.4."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news