NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema, hadi Aprili 2024, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya jumla ya shilingi trilioni 21.3 sawa na ufanisi wa asilimia 96.9 ya lengo la Julai 2023 hadi Aprili 2024 na asilimia 79.8 ya lengo la mwaka.
Ameyasema hayo leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.
Dkt.Nchemba amesema, katika kuimarisha na kuboresha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato,mamlaka imeanza ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) ambao ni mahsusi kwa usajili, ukadiriaji, ukusanyaji wa kodi na ufuatiliaji wa walipakodi.
"Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kutekeleza mradi wa kuunganisha mifumo ya ndani na taasisi nyingine za serikali ikiwemo mfumo wa kuzalisha vitambulisho vya Taifa-NIDA na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni-BRELA.
"Na kuboresha moduli ya lango la huduma kwa mlipakodi na moduli ya uwasilishaji wa ritani za kieletroniki kwa mapato ya ndani."
Waziri Dkt.Nchemba amesema, hatua zilizochukuliwa kudhibiti uvujaji na upotevu wa mapato ni pamoja na kuanzisha divisheni mpya ya walipakodi wa kati na wadogo chini ya Idara ya Kodi za Ndani.
Pia, kuimarisha mifumo ya kubadilishana taarifa na wadau wa ndani na nje ya nchi, kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya vitendo vinavyoashiria ukwepaji kodi.
Sambamba na kuendelea kuhamasisha wananchi kuhusu masuala ya kodi hususani umuhimu wa kudai na kutoa risiti za kielektroniki (EFD) na matumizi na uhakiki wa stempu za kielektroniki (ETS).
"Aidha, mamlaka imetoa elimu ya kodi kwa walipakodi kupitia njia mbalimbali ikiwemo semina, vipindi vya redio na televisheni, matangazo ya kodi, mikutano ya wadau wa kodi, kampeni, mitandao ya kijamii na vipeperushi."
Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, hadi Aprili 2024, Bodi ya Rufani za Kodi imepokea mashauri ya kodi 437 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 3,456.5 na imesikiliza na kutolea uamuzi mashauri 388 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 2,780.1 na dola za Marekani 439,281.
Aidha, Baraza la Rufani za Kodi limesajili jumla ya mashauri 112 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 2,790 ambapo mashauri 64 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 137.9 yamesikilizwa na kutolewa maamuzi na mashauri 56 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 2,510 yako katika hatua mbalimbali za usikilizaji na kutolewa maamuzi.
Vilevile, Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imepokea malalamiko 40, imesuluhisha malalamiko 22 na malalamiko 18 yapo katika hatua mbalimbali za usuluhishi.
"Kadhalika,taasisi imeanzisha mfumo wa kupokea malalamiko kwa njia ya simu (call center) ambapo mlalamikaji au mtoa taarifa anaweza kuwasilisha malalamiko kwa kupiga simu ya bure namba 0800111022."
Amesema,jitihada hizo zimewezesha ongezeko la mwamko wa wananchi na walipakodi kuwasilisha malalamiko yao kwa uhuru na uwazi.
"Ili kuhakikisha walipakodi wanakuwa na uelewa na kunufaika na huduma zinazotolewa, Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imeendelea kujitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
"Ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na wahariri wa vyombo vya habari na vikundi vya wafanyabiashara katika Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uwepo wa ofisi, majukumu yake na namna ya kuwasilisha malalamiko."
Waziri Dkt.Mwigulu amesema, pia taasisi hiyo imeshiriki katika mikutano mbalimbali ya umoja wa wafanyabiashara katika mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Mbeya, Mtwara, Lindi na Dar es Salaam kwa lengo la kutoa elimu ya usuluhishi wa masuala ya kodi.