NA LWAGA MWAMBANDE
UPENDO ndiyo amri kuu ambayo kila mmoja wetu anaalikwa kuuishi katika maisha yake.
Picha na The Sun Nigeria.
Aidha,tunaendelea kuishi vizuri kwa sababu ya kuishi upendo hata sisi kuwepo duniani ni upendo wake Mungu mwenyewe. Hakuna aliyewahi kuomba kuzaliwa bali tumezaliwa kwa upendo wa asili.
Miongoni mwa machapisho ya mtandaoni kutoka kwa Mwalimu Deogratius Kessy anabainisha kuwa, tunapojifunza mambo ya familia ni kwa sababu sisi wote tumezaliwa katika familia ambazo tunazo leo.
Na katika familia huwa kuna watoto na ndiyo maana tunajifunza malezi ya watoto.
Vile vile, watoto huwa wanajifunza sehemu kubwa ya makuzi yao kutoka kwa wazazi.
Pia,wanajifunza namna bora ya kuwa mama kutoka kwa mama na namna bora ya kuwa baba kutoka baba.
Hata miito mingine chimbuko lake ni katika familia, hivyo tukiweza kuwa na familia bora basi tutaweza kuwa na jamii bora. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema kuwa,siku zote tukiwapenda watoto, basi tunajipenda wenyewe.Endelea;
1. Mimi napenda watoto, wewe ndugu yangu vipi?
Ninapenda wapate joto, siwaze walale wapi,
Yabaki kwangu mapito, wao wabakie hapi,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
2. Siku hii ya mtoto, hapa kwetu Afrika,
Kumbukumbu yake nzito, ya kusini mwa Afrika,
Waliuliwa watoto, mateso yakasikika,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
3. Bila watoto ni ndoto, kuendeleza kizazi,
Tutakwenda kama mto, kukauka kiangazi,
Sawa kushika mfuto, kukimaliza kizazi,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
4. Waende shule watoto, hata sisi tujinyime,
Tusikilizie wito, kutaka wao wasome,
Tusiwakawize watoto, kwa pendo tuwatazame,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
5. Wakigonjeka watoto, peleka zahanatini,
Kama linazidi joto, nenda hosipitalini,
Wapate tiba watoto, washamiri duniani,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
6. Mahitaji ya watoto, ni mengi tunayaweza,
Wape furaha watoto, bila ya kuwapoteza,
Mzazi kuwa mvuto, wao ukiwapendeza,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
7. Kuharibika watoto, wazazi tunachangia,
Utukututu wa watoto, walezi tunachangia,
Bila malezi watoto, shimo tunawachimbia,
Tukiwapenda watoto,tunajipenda wenyewe.
8. Unyanyasaji watoto, tuache si jambo zuri,
Kutelekeza watoto, sawa sawa na sifuri,
Sote tufanye watoto, wasipate yote zari,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
9. Kuwaharibu watoto, kwa sababu sio wako,
Ujipatie kipato, na faida iwe yako,
Ninasema kwa mkato, iache tabia yako,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
10. Sote tulee watoto, kama twazaa wenyewe,
Wasiwekwe kwenye moto, twajimaliza wenyewe,
Tuwajenge kwa kipato, watatufaa wenyewe,
Tukiwapenda watoto, tunajipenda wenyewe.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602