Tume ya TEHAMA kujenga maabara ya kwanza ya vifaa vya kieletroniki ndani ya TIRDO

NA GODFREY NNKO

TUME ya Tehama nchini (ICTC) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) zimesaini Mkataba wa Maelewano (MoU) kwa ajili ya kujenga Maabara ya Kutengeneza, Kukarabati na Kuunganisha Vifaa vya Kieletroniki nchini.
Maabara hiyo ya kisasa ambayo inatarajiwa kujengwa na tume ndani ya shirika hilo inatarajiwa kuwa fursa kubwa kwa vijana kustawisha bunifu zao nchini.


Pia, taasisi hizo za umma zitashirikiana katika sekta zingine kama kuunganisha vifaa vya kielektoniki, kufanya matengezo vifaa vilivyoharibika.

Vile vile kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wataalam wa TEHAMA na kuhuisha vifaa vilivyokwisha muda wake ili viweze kuingia sokoni tena kwa matumizi.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Juni 7,2024 makao makuu ya TIRDO jijini Dar es Salaam ambapo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA,Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga na Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO,Prof.Mkumbukwa Madundo Mtambo ndiyo waliosaini kwa niaba ya taasisi zao.

Tume ya TEHAMA

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA,Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga amesema, makubaliano hayo yanakwenda kuimarisha Sekta ya TEHAMA nchini, ikizingatiwa kuwa TIRDO ni taasisi kongwe yenye uwanda mpana katika eneo la tafiti za viwanda.
Amesema, tume hiyo ina majukumu mawili ikiwemo kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA na kukuza TEHAMA.

Dkt.Mwasaga ameongeza kuwa, TIRDO wana uwezo mkubwa wa kupima vifaa na kusimamia ubora wa vifaa ambavyo vitatengenezwa kwenye TEHAMA.

"Katika kukuza TEHAMA, tunakuza wataalamu, tunakuza wajasiriamali ambao wanakuwa na Startups, tunakuza uchumi wa Kidigitali wa mikoa yote ya Tanzania na vile vile kuifanya Tanzania iwe shindani kwenye uchumi wa kidigitali wa Dunia.
Kwa hiyo haya majukumu mawili yana maana kubwa sana, hiki tunachokifanya leo.

Napenda nikubaliane na Profesa, ni kitu cha aina yake kwa sababu katika ubunifu mkubwa ambao unafanyika Tanzania kwa kawaida, tumeona kuna mafanikio makubwa tumefanya sana katika eneo la kutengeneza mifumo au softwares.

Katika kufanya ubunifu ambao unahusisha bidhaa za TEHAMA, hilo ni eneo ambalo tunahitaji kulifanyia kazi vizuri zaidi.
Kwa hiyo, hii ni hatua moja wapo ya kuhakikisha kwamba tunafikia kuwa nchi ambayo siyo tu inauza mifumo ya software, lakini tufikie hatua kwamba tunauza bidhaa za TEHAMA katika masoko ya ndani ya nchi, masoko ya kikanda na masoko ya Kiafrika.

Wote, tunafahamu sasa hivi Tanzania ipo katia Soko Huru la Afrika na katika soko hilo kuna ushindani mkubwa.

Na sisi tunaamini kabisa, tukifanya bunifu zetu ziweze kufanikiwa vizuri hasa kwa kushirikiana na taasisi kama hii ya TIRDO kwa sababu TIRDO yenyewe ina strengths kubwa ya kusapoti research.

Wabunifu wengi kwa ubunifu wao peke yao, unaweza kukuta ana uwezo wa kubuni, lakini sehemu ya kufanya tafiti ambayo inahusiana na vitu hivyo inakuwa kidogo gharama kubwa, au itamfanya huyo mbunifu ashindwe kufanya mambo.
Kwa hiyo, kwa kushirikiana na taasisi kama TIRDO inatuongezea nguvu katika majukumu yetu.

Moja wapo ya jukumu la tume ni kufanya tafiti, kufanya tafiti katika eneo la TEHAMA wote mnafahamu kabisa Tume ya TEHAMA ndiyo msimamizi wa sekta ya Tehama nchini,na hakuna sekta ambayo inaweza kukuwa bila kuwa unafanya tafiti.

Tafiti zinabadilishwa kuwa teknolojia, teknolojia inazaa innovation then unakuwa na makampuni mbalimbali.

Kwa hiyo mahusiano haya ni mahusiano ya kistratejia ni mahusiano ambayo yatawasaidia sana wabunifu wetu wa Tanzania.
Na itatuongezea tija kubwa, kwa sababu wote tunafahamu katika ubunifu wa TEHAMA duniani, wanaofanikiwa ni wale ambao wanafanya ubunifu uliobebwa na tafiti.

Na tafiti ambazo kwa sasa hivi zinaonekana kwamba zina tija kubwa ni zile zinazohusisha bidhaa za TEHAMA.

Kwa mfano, nadhani mmeona katika Dunia hii ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence), vitu vinavyouzika vingi ni bidhaa ambazo zina akili.

Ninadhani, wote mliona kuna roboti (Eunice) aliletwa hapa na tulimuona alivyo yule roboti part moja ni software, parts kubwa ni hardware.
Kwa hiyo vyote vinafanyika kwa pamoja ili kuweza kutengeneza vitu kama hivyo, ni kwenye maabara kama hii ndiyo tutaweza kuzalisha bidhaa za namna hiyo.

Kwa sababu TIRDO ana vigezo vyote, ana wabunifu ambao wapo ndani kama katika hub hii tuliyopo (Tirdo Hub) hapa.

Wana uwezo mkubwa wa kupima vifaa na kusimamia ubora ya vifaa ambavyo vitatengenezwa kwenye TEHAMA.

Kwa hiyo, sisi kama tume tuna furaha kubwa sana kwa siku ya leo. Na ningependa kuwapa shukrani timu nzima iliyohusika kutoka TIRDO na Tume ya TEHAMA.

Sisi katika majukumu yetu, tunategemewa sana kufanya kazi na taasisi mbalimbali za Serikali, ndiyo maana jukumu moja wapo inasema tume inatakiwa itengeneze hali ambayo kazi zetu ambazo tunazifanya ziwe na mahusiano na taasisi nyingine.

Kwa hiyo, hiki ambacho tunakifanya leo ni kitu ambacho kipo ndani ya majukumu yetu.Sisi tunatakiwa tuchagize, ili kufanya mambo yaweze kufanikiwa.

Katika masuala ya Mapinduzi ya Kidigitali (Digital Transformation), sisi kwa Tanzania tunaangalia nguzo tano.
Nguzo moja wapo ni kuwapa ni kuwapa watu ujuzi wa mambo ya TEHAMA (Digital Skills).

Pili ni kuhakikisha kwamba, hiyo mifumo au bidhaa tutakazotengeneza hapa ziwe zina usalama, na zinaweza kuaminika kwa watumiaji.

Tatu, ni kuhakikisha kwamba huduma za mawasiliano zinawafikia watu wote bila ubaguzi wowote.

Nguzo ya nne ni Nguzo ya Uchumi wa Kidijitali, nadhani mnatambua sasa hivi kuna document ambayo inaonesha mambo ambayo tutayafanya katika kuujenga uchumi wa kidigitali.

Na nguzo ya tano ambayo inahusiana na utafiti, ujasiriamali na ubunifu ambao sasa hiki kituo ndiyo kitafanya kazi kubwa sana katika eneo hilo,"amefafanua kwa kina Dkt.Mwasaga.

Amesema, mahusiano ya taasisi hizo mbili za umma yanatarajiwa kuwa ya muda mrefu ili kuyafikia makundi ya vijana wote nchini.

TIRDO

Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof.Mkumbukwa Madundo Mtambo amesema,wamefikia makubaliano hayo ya kuanzisha maabara hiyo ili kuhakikisha wataalam wanapata sehemu ya kupata ujuzi na kuandaa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya sekta mbalimbali nchini pamoja na viwanda nchini.
"Tunashukuru sana wezetu wa Tume ya Taifa ya TEHAMA kuona kuwa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwamba ni sehemu muafaka kwa kushirikiana katika suala hili muhimu kwa Taifa letu.

Pili, niseme kwamba nimefarijika kutenga muda wenu kwa kuona leo yafanyike haya makubaliano, mahali ambapo mnataka kuanzisha hiyo maabara kwa maana ya TIRDO.

Lakini, niwashukuru wote ambao wameandaa mchakato mzima mpaka tumefikia hatua hii, kwa ajili ya kuanzisha hiyo maabara.

Niwapongeze sana wote kwa upande wa TIRDO na Tume ya Taifa ya TEHAMA na niwaombe tuendelee na juhudi hii ambayo mmeianzisha mpaka tufikie hatua kuona kwamba kimesimama na kinafanya shughuli ambayo imepangwa kufanyika.

Ni matumaini yangu kwamba kwa kuanzishwa kituo hiki kitasaidia viwanda ambavyo vinatumia vifaa vya kieletroniki, lakini wajasiriamali mbalimbali.
"Lakini vile vile na kuhaulisha teknolojia na vile vile kuleta ajira hasa kwa vijana wetu wabunifu, kwa hiyo hiki ni kitu ambacho kwa Taifa letu ni muhimu sana kwa shirika, lakini kwa nchi kiujumla,"amesisitiza Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof.Mkumbukwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news