Tume ya TEHAMA, SIDO waja na neema mpya kwa vijana Uchumi wa Kidijitali

NA GODFREY NNKO

TUME ya TEHAMA nchini (ICTC) imeingia makubaliano na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogovidogo Tanzania (SIDO) ili kufanikisha vituo vya ubunifu ambavyo vitawasaidia vijana kuweza kukuza kampuni zao za ubunifu nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Juni 6,2024 katika ofisi za SIDO makao makuu jijini Dar es Salaam ambapo kwa kuanzia, mameneja wa mikoa sita wa SIDO wamesaini mikataba na tume kwa ajili ya utekelezaji huo.
Aidha, mameneja waliosaini mkataba na tume ni kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mbeya, Mwanza na Lindi.

Tume ya TEHAMA

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Mkundwe Moses Mwasaga amesema, makubaliano hayo ya kihistoria yamelenga kuwezesha vijana wa Kitanzania kuneemeka kupitia Uchumi wa Kidijitali.
"Leo hii sisi tunafurahi sana, kwa hii shughuli tuliyofanya ya kusaini hayo makubaliano sita ya mikoa sita katika programu kubwa, ambayo tunapanga hiyo programu ifike Tanzania nzima."

Dkt.Mwasaga amesema,programu hii imelenga vijana na wanachofanya, wamekubaliana na wenzao SIDO.
"Kwa sababu SIDO ndiyo incubator na acceleretor ya kwanza Tanzania.Na ndio kubwa na ndio yenye maeneo mikoani kote, sisi tunachofanya nao ni kwamba tunajenga vituo vya ubunifu."

Amesema, vituo hivyo vya ubunifu vitawasaidia vijana kuweza kukuza kampuni zao za ubunifu nchini.

"Tume, katika moja ya kazi yake katika kukuza TEHAMA Tanzania ni kuhakikisha kwamba, Tanzania inakuwa na uchumi wa kidigitali ambao huo uchumi unakuwa unajengwa na kampuni ndogo ndogo nyingi za vijana.
"Kwa hiyo mahusiano yetu na wao ni mahusiano ambayo yote tunaongezeana nguvu katika kuhakikisha kulifanikisha hilo."

Aidha, kuhusu vijana wangapi ambao watahusika na jambo hilo, Dkt.Mkundwe amesema, "TEHAMA kama mnavyoifahamu ina watu wa aina mbili ukiondoa watumiaji.
"Kuna kampuni ambazo zinatumia TEHAMA ili kufanya shughuli anayoifanya iende vizuri zaidi.

"Ni kama hao ambao mnaona wanatumia Instagram na vitu vingine, halafu kuna kampuni zingine zenyewe biashara yake ndiyo TEHAMA.
"Sasa hao wote ni wanufaika wa hivi vituo tunavyovijenga. Na tumeanza na vituo sita na ukiondoa hivyo sita, viwili ambavyo vitakuwa katika mikoa hiyo hiyo ni vituo vya kutengeneza bidhaa za TEHAMA.

"Kwa hiyo, hapa tunaangalia tu kwamba siyo suala la kutengeneza kampuni ambalo tutatengeneza mifumo tu, lakini tutazisaidia kampuni ambazo zitakuwa zinatengeneza vifaa vya TEHAMA.
"Na hilo linaendana na adhima ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba tunaujenga uchumi wa kidigitali wa Tanzania ambao unakuwa define na kampuni za vijana.

"Kwa sababu wote tunafahamu kwa Tanzania sasa hivi, vijana tulio nao ni takribani milioni 21 kutokana na Sensa tuliyofanya iliyopita."Amesema, hao vijana wanatakiwa wawajengee uwezo wa kibunifu ili waweze kutengeneza makampuni.

Dkt.Mwasaga amesema,wakitengeza hayo makampuni yatakuwa yanafanya vitu viwili vikubwa ambavyo tume imeundwa kwa ajili yake.

"Cha kwanza kutengeneza ajira kwa vijana na cha pili kufanya Sekta ya TEHAMA iweze kutoa mchango mkubwa kwenye Pato Kuu la Taifa la Tanzania.Kwa hiyo hayo ndiyo mambo ambayo tunayaangalia."
Amesema, gharama za vituo hivyo sita ambayo inahusiana na ukarabati wa maeneo na pia kuweka vifaa vinavyotakiwa ni zaidi ya shilingi bilioni 8 za Kitanzania ambazo zitahusika katika mambo hayo.

"Na huu mradi utaenda nchi nzima ili tuweze kuhakikisha kwamba, vijana wanakuwa na chachu ya kuanzisha makampuni, kwa sababu wote sasa hivi tunafahamu kuna soko huru la Afrika ambapo Tanzania sasa hivi ni mwanachama.

"Tunataka hawa vijana wetu, bunifu zao zieweze kupata masoko Afrika nzima ikiwezekana na vile vile waweze kushindana duniani.

"Kwa hali ya sasa hivi, nadhani wote mnafahamu mifumo mingi tunayoitumia hasa kwenye masuala mfano ya mitandao ya kijamii na vitu vingine haikutengenezwa Tanzania.
"Kwa kutumia hivi vituo, tutawapa ujuzi vijana, tuweze kutengeneza mifumo yetu ya Kitanzania, tuweze kupata soko la hapa na soko la nje.

"Na wote, sisi tunafahamu kabisa Tanzania sisi kwenye ushindani tuna bahati, Kiswahili kimewekwa katika lugha za Afrika, kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kutengeneza mifumo mbalimbali ambayo itakifanya Kiswahili kiweze kutumika sehemu mbalimbali.

Hiyo hizo ndiyo sehemu ambazo tutakuwa tunafanya hivyo, tunaprogramu mbalimbali tunaweza kuwakutanisha watu wa mabenki, watu wa kisheria, watu wa kutengeneza kampuni na vitu vingine ili kuwasaidia hawa vijana waweze kuanzisha kampuni nyingi ili tuweze kujenga uchumi wa kidigitali ambao ni shindani kwa Tanzania."

SIDO

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji amesema, makubaliano hayo na tume yamewapa faraja kubwa katika kulifikia kundi kubwa la vijana nchini.
"Leo hii tumefarijika kuingia makubaliano na Tume ya TEHAMA kwa madhumuni ya kuanzisha vituo mahiri vya TEHAMA.

"Tutakuwa na vituo sita vya kwa kuanzia ambavyo ni vya ubunifu ambapo tutakuwa na vituo viwili ambavyo vitakuwa ni kwa ajili ya ukarabati wa vifaa hivi vya TEHAMA.

"Tunaanza na mikoa hii sita, lakini katika kuanzisha hiki tunatarajia vijana watakuwa wanaingia katika sehemu zetu wanapata mafunzo, wanafanya kazi za ubunifu.

"Lakini, baada ya muda wanaondoka, wakiondoka wanaingia vijana wengine, kwa hiyo kwa maana hiyo tunatarajia kuna viwanda vingi vitaanzishwa ambavyo vitakuwa vinahusika katika ukarabati wa vifaa vya TEHAMA.

Lakini, vile vile huko mbeleni ambako tunaenda tunatarajia basi, tutakuwa na vijana ambao wataanzisha viwanda vya kutengeneza vifaa vya TEHAMA.

Kwa hiyo, simu ambazo tunaziona sasa hivi zinatengenezwa kutoka nje, tunategemea basi kwa miaka ijayo tutakuwa tunahakikisha zinatengenezwa hapa Tanzania.

Kwa hiyo ni fursa kubwa kwa vijana kwa sababu wataweza kujiajiri, lakini fursa kubwa kwa Serikali kwa sababu tutakuwa na vijana ambao wamejiajiri ambao tayari watakuwa wamerasimisha kazi zao.

Hivyo, kuweza kulipa kodi kwa nchi. Kwa hiyo, nchi yenyewe itafaidika, lakini vijana wenye watafaidika.
"Kwa hiyo, tutaendelea kuwa katika Dunia ambayo inaenda na TEHAMA kumbuka tuko katika Dunia ambayo bila TEHAMA kwa kweli utaachwa mbali sana.

Lakini, kwa makubaliano haya sasa tunaona kabisa vijana au Watanzania wanaingia katika Dunia hii ya TEHAMA, hivyo kwenda kushindana lakini vile vile kwenda na wakati."

Amesema, mradi huo ambao unaanza unatarajiwa kuwa endelevu huku vijana wengi nchini wakinufaika nao.

"Kwa sababu ni endelevu, tutaanza na vijana wachache lakini kadri siku zinavyoenda vijana watazidi kuongezeka, kwa maana kwamba watakuwa wanaingia, wakishapata ule ujuzi wataweza kuondoka na kufungua makampuni yao, lakini vile vile kutakuwa na vijana watakuwa wanaingia na wengine wanatoka.

"Kwa hiyo ni kituo hatamizi ambapo wanajifunza na kuondoka, lakini wanajifunza kwa kufanya kazi kwa vitendo."

Amesema, watekelezaji wa mradi huo ni Tume ya TEHAMA, lakini SIDO watakuwa wanatoa maeneo kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati na tume ikiwemo kuleta vifaa vyote.

"Kwa hiyo, sisi tutawaleta vijana wetu waweze kuingia katika sehemu husika na baada ya ujuzi watawapisha wengine, kwani tayari watakuwa na uwezo wa kuanzisha vituo vyao."
Pia, amesema walengwa ni vijana wote bila kujali elimu au kiwango cha elimu alicho nacho.

"Sifa kubwa awe ni kijana Mtanzania basi, anaweza akawa amesoma sana au hajasoma sana, lakini ni kituo ambacho mtu anaweza akakitumia kwa ajili ya ujuzi."

Lindi

Frida Mungulu ambaye ni Meneja wa SIDO Mkoa wa Lindi amesema,heshima waliyopata kuotoka tume kufanikisha vituo vya ubunifu inakwenda kuleta matokeo chanya kwa vijana wabunifu nchini.
"Tumesaini makubaliano haya na Tume ya TEHAMA na lengo kuu ni katika kuhamasisha na kuibua vijana ambao wataingia kwenye programu hii ya kuwaatamia katika mambo ya TEHAMA kwa ujumla.

"Ili waweze kuwa makini kama ni kufanya ukarabati au kuendeleza programu mbalimbali kwa lengo la kuleta chachu katika uchumi kwa ujumla.

"Lengo letu, kwanza kabisa kuzalisha ajira kwa vijana kwa sababu tunafahamu tuna vijana wengi hawana ajira, wamesoma lakini wako mitaani.

"Lakini, pia Sekta ya TEHAMA iweze kuchangia katika pato la Taifa.Kwa hiyo, sisi SIDO kama walezi na wasaidizi wa kusaidia Serikali katika kuendelea na kuanzisha viwanda vidogovidogo na hasa biashara ndogo na za kati.
"Ni jukumu letu kuwalea vijana katika viatamizi ambavyo ni Incubation Centres, tutakuwa na hizo ICT hub katika mitaa yetu ya viwanda kwa ajili ya kulea mawazo ya hao vijana, watafundishwa na watapewa huduma wezeshi ili waweze kuiva na kuwa mafundi mahiri au wafanyabiashara wazuri ili waweze kuwasaidia vile vile vile wafanyabiashara ndogo ndogo na wa kati na hasa wazalishaji."

Arusha

Naye Jafari Donge ambaye ni Meneja wa SIDO Mkoa wa Arusha amesema,makubaliano hayo yanakwenda kuwa na tija kubwa kwa vijana Arusha.

"Tumesaini mkataba wa makubaliano. Lakini, baada ya kusaini mkataba huu katika mkoa wetu wa Arusha kitajengwa kituo ambacho kitakuwa na components mbili, cha kwanza ni kwa ajili ya ubunifu.
"Halafu cha pili utakuwa ni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Tehama, mkoa wetu wa Arusha una vijana wengi sana, tuko na vyuo zaidi ya vinne pale.

"Na bahati nzuri sisi Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo katika Mkoa wa Arusha tumeingia mkataba na vyuo.

"Kama Chuo cha Uhasibu ambacho kina wanafunzi zaidi ya 10,000. Kuna Chuo cha Ufundi, Arusha Techinical College kwa hiyo vijana wanapohitimu pale kwa kupitia kituo cha kwetu, ina maana kwanza watakuja kujifunza pale bunifu mbalimbali zitakazoweza kutoa masuluhisho kwa matatizo ya kidigitali na kujenga ajira mbalimbali kwa vijana na katika kukuza uchumi wa Taifa letu.
"Kwa hiyo, pale vijana watakuwa wanakuja wanatengeneza vifaa mbalimbali vya TEHAMA pale ambavyo tutakuwa tunaviingiza sokoni.

Na kwa kufanya hivyo, kwanza gharama ya vifaa vya TEHAMA katika mkoa wetu, bei itakwenda chini mfano kama kompyuta, simu wanaweza kutengeneza kwa hiyo gharama itakuwa nafuu katika mkoa wetu na itawawezesha vijana kusoma vizuri na sisi kwenye viwanda vile vile tunategemea tutapata teknolojia mbalimbali ambazo zitakuwa ni rafiki katika uendeshaji wa mashine zetu.

"Tumekuwa tukitumia mashine ambazo zina teknolojia za zamani, ni mannual lakini sasa hivi vijana watakuja na bunifu ambazo zitatusaidia kurahisisha utendaji kazi kwa teknolojia tuliyonayo na ya sasa hivi mpya wataweza kufanya kazi vizuri."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news