DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Watanzania wanaojishughulisha na masuala ya uwekezaji na kuweka mazingira wezeshi ili kuwasaidia wawe mahiri.
Amesema kuwa, sera za uwekezaji nchini zinatoa unafuu kwa watanzania kuingia kwenye uwekezaji na Serikali itaendelea kufanya maboresho ili wapate nafasi ya kuwekeza.
Amesema hayo leo Alhamisi Juni 13, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni, Dodoma.
Mbunge huyo alitaka kujua mikakati ya Serikali ya kuboresha sera ili zitoe upendeleo maalum kwa wazawa na waweze kushiriki kujenga uchumi endelevu.
“Si hilo tu, tunayo sera ambayo tumeitengenezea sheria ya ‘Local Content’ kwa miradi mikubwa ambayo inatekelezwa kama mradi wa kuzalisha Umeme wa Maji wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya SGR na miradi mingine ya kimkakati tumeweka kipengele kutengeneza fursa za watanzania kushiriki kwenye ujenzi.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inafanya upembuzi na tathimini ya kutambua wawekezaji ambao wameshindwa kuendeleza viwanda na mashamba waliyokabidhiwa na Serikali ili kuyarejesha na kuwapa wawekezaji wengine wenye uwezo ya kuyaendeleza.
“Tathimini inayofanywa na Wizara ya Kilimo itawezesha Serikali kuchukua maamuzi ya kuyarudisha maeneo haya ili kuyaendeleza au kumpatia mwekezaji mwingine anayehitaji kuwekeza.”
Amesema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava ambaye aliishauri Serikali ifanye tathimini ya kina kwa viwanda na mashamba ambayo yalibinafsishwa na hayaendelezwi mpaka sasa ili kuokoa uchumi wa nchi na kuwasaidia wananchi.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo ifuatilie maeneo ambayo bado hayajaanza kutumia mfumo wa minada katika kuuza mazao ya wakulima hasa kwenye mikoa na wilaya ambayo ina Vyama vya Ushirika.
“Mfumo wa mnada unawezesha wakulima kupata bei nzuri ya mazao yao, na umeonesha mafanikio tangu tulipoanza kuutumia.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa kufuatilia katika ngazi ya Wilaya ambako vyama vya ushirika vipo ili kujiridhisha iwapo mazao yanauzwa kwa njia ya mnada.
“Kama hawauzi kwa njia ya mnada mjue ni kwa nini wakati mnada ndiyo inatoa fursa kwa wakulima kuuza kwa bei nzuri.”
Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate ambaye alitaka kujua kauli ya Serikali kwa maeneo ambayo hayajaanza kuuza mazao kwa njia ya mnada.