DAR-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) imesema kuwa, itaanza kuwashughulikia ipasavyo wapiga kura wanaodhani kwamba uchaguzi ni fursa ya kupata manufaa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao wa 2025.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo Juni 27,2024 na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Neema Mwakalyelye kwenye warsha ya siku moja iliowashirikisha viongozi mbalimbali wa dini hapa nchini kwa lengo la kujadili na kuweka mkakati wa kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
"Tumefutilia miaka ya nyuma katika chaguzi tulijikita kwa wagombea ambao ndio walikuwa na ushawishi mkubwa wa rushwa, lakini sasa kuna aina mpya ya rushwa,hivyo tumepanua wigo mkubwa zaidi kwa wapiga kura kwa kuwa inaonesha wao ndio wamekuwa wakishawishi wagombea kutoa rushwa," amesema.
Amesema kuwa, kwenye chaguzi za hivi karibuni wamebaini kwamba wapiga kura ndio wamekuwa wakidai wapatiwe manufaa ili waweze kuwachagua viongozi jambo ambalo linaweza kusababisha athari.
Amesema,wapiga kwa sasa wanaona uchaguzi ni fursa ya wao kupata manufaa, "hawajui kwamba wanauza haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi na hivyo inaweza kuleta hatari kwa kuwa tutaishia kupata viongozi waliochaguliwa katika mfumo halali.
"Lakini kwa njia isiyo halali inayotokana na rushwa na kufanya viongozi hao kutowajibika ipasavyo kwa sababu waliwekeza kwenye kutoa rushwa na hivyo kuishia kufanya kazi kwa kujinufaisha wao na si wananchi."
Aidha, amewaomba viongozi wa dini kutilia mkazo kwa kuwasisitiza waumini wao wawapo kwenye nyumba za ibada kuepukana na vitendo vya rushwa ili kubadilisha taswira ya Taifa.
Amesema, viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana ya kubadilisha jamii na kwamba,
"Kama mnavyofahamu mwaka huu 2024, tutakuwa na Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa na mwakani, 2025, tutakuwa na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
"Vitendo vya rushwa katika uchaguzi vinasababisha kuwa na uchaguzi usiozingatia misingi ya haki na usawa; na hili limekuwa ni tatizo la kidunia ambapo hata Tanzania haijaachwa salama."
Kwa upande wake,Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Alex Malasusa, ametoa wito kwa watanzania kutoshiriki vitendo vya rushwa iwe katika chaguzi au baada ya uchaguzi na kwamba kila mtanzania awe wazi kutaja aliyetoa au kupokea rushwa ili wote washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Amesema, watu ni mafundi wa kuongelea rushwa kila kukicha, lakini bila kuwa na utashi ni kazi bure na kusisitiza kwamba utashi ukiambatana na vitendo unahitajika zaidi.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani, Alhad Mussa Salum amewapongeza viongozi wa TAKUKURU kwa dhamira yao njema ya kuwashirikisha viongozi wa dini katika harakati za kuzuia na kupambana na rushwa.
Aidha,aliwaomba viongozi hao kuangalia uwezekano wa kufanya kongamano kubwa na kuwaalika viongozi wengi wa dini kwa kuwa wapo wengi zaidi.
Tags
Habari
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania
Uchaguzi Mkuu 2025
Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024