Ujangili, uharibifu misitu unafifisha maendeleo-Jaji Mkuu Profesa Juma

DAR-Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 19 Juni, 2024 amefungua kikao kazi cha wadau wa haki jinai ili kujadili changamoto zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anafungua kikao kazi cha wadau wa haki jinai ili kujadili changamoto zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu leo tarehe 19 Juni, 2024 jijini Dar es Salaam.

Kikao kazi hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Crown Plaza jijini Dar es Salaam kimewaleta pamoja wakuu mbalimbali wa vyombo vya haki jinai nchini, ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kikosi cha Kupambana na Ujangili na Wakala wa Misitu Tanzania.

Wengine walioshiriki kikao kazi hicho ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Maafisa kutoka PAMS Foundation, akiwemo Mkurugenzi wa Uendeshaji na Mafunzo, Bw. Samson Kasala.Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi hicho, Mhe. Prof. Juma alisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na kueleza hatari ya matumizi mabaya ya wanyamapori na kupoteza misitu, jambo ambalo baadaye linaweza kuharibu mazingira na kupoteza uhai wa binadamu.

“Hili ni jambo la msingi ambalo linatuunganisha wote. Wanyamapori na misitu yetu inapotea kutokana na biashara yenye faida kubwa ambayo inasukumwa na nchi za nje zaidi kwenye masoko na kuharibu ikolojia yetu. Kwa hiyo, kukutana kuangalia jinai zinazotokana na makosa ya wanyamapori na misitu ni jambo ambalo ni muhimu linalotuunganisha,” amesema.
Jaji Mkuu ameeleza jambo lingine linalowaunganisha wadau ni ukweli kwamba faida haramu inayotokana na matumizi mabaya ya wanyamapori na misitu na fedha zinazopatikana zinatumika katika mambo ya ugaidi, ambayo yanaweza kutikisa usalama na maendeleo ya nchi zinazoendelea.

“Hivyo, huu mkutano una faida kubwa zinazoonekana. Nichukue fursa hii kuwasilisha shukrani zangu kwa PAMS Foundation ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kutoa msaada wa fedha na hali kuwezesha mafunzo mbalimbali kufanyika,” Mhe. Prof. Juma amesema.
Mratibu wa kikao kazi hicho, Mhe. Raymond Venance Kaswaga akitoa utambulisho wa washiriki na Viongozi waliohudhuria kabla ya ufunguzi.

Amebainisha kuwa kulifanyika uchunguzi mwaka 2022, baadaye mafunzo yakafanyika mwaka huo wa 2022, 2023 na 2024 ambayo yamewasaidia wengi katika kutekeleza sheria mbalimbali ambazo zinasaidia kuweka mizani sawa kati ya kulinda wanyamapori na misitu na haki binafsi za wananchi.

Jaji Mkuu akasisitiza lazima mizani ipatikane kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na haki zao, lakini vile vile wanyamapori na misitu inalindwa kwa faida kubwa ya nchi.
Sehemu ya washiriki wa kikao kazi hicho (juu na chini) wakifuatilia hotuba ya ufunguzi iliyokuwa inawasilishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha).

Kwa upande wa Mahakama, Mhe. Prof. Juma amesema wanakubaliana na dira na malengo makubwa ya PAMS Foundation ya kuwawezesha wananchi na Taasisi zinazolinda wanyamapori, misitu na mimea ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.

“Vilevile tunakubaliana na malengo makuu ya kuwezesha wananchi kufahamu faida kubwa inayotokana na ulinzi wa wanyamapori na umuhimu wa mwingiliano baina ya wanyamapori na binadamu kwa sababu binadamu hawezi kubaki na usalama wowote ukiondoa wanyamapori na misitu,” amesema.

Amekishukuru Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kuweza kuwakusanya pamoja wadau muhimu katika maeneo hayo ya wanyamapori na misitu, jambo ambalo linaimarisha ushirikikiano kwa malengo ya pamoja katika kulinda mazingira, wanyamapori, misitu na haki za binadamu.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kufungua kakao kazi hicho.

Naye Mkuu wa Chuo cha IJA na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo, katika maelezo yake ya awali aliishukuru PAMS Foundation iliyowakilishwa na Bw. Kassala na Mkurugenzi wa Upelelezi na Uchambuzi, Bw. Elisifa Ngowi, kwani ushirikiano na msaada wao umekuwa muhimu katika kuongeza uwezo wa kutatua changamoto zinazotokana na makosa ya wanyamapori na misitu.

Alibainisha kuwa programu za mafunzo na mipango ya pamoja waliyoanzisha ni ushuhuda wa kile kinachoweza kufikiwa kwa pamoja.

Mhe. Dkt. Kihwelo alieleza kuwa kikao kazi kilichoandaliwa ni hatua muhimu kuelekea kutengeneza mikakati inayotekelezeka na kuimarisha mifumo ya utekelezaji ya kimahakama.

“Ninawaalika kila mmoja wenu kushiriki kikamilifu katika mijadala, kushiriki ufahamu wenu na kuchangia katika kuunda mustakabali wa utekelezaji wa sheria ya makosa ya wanyamapori na misitu nchini Tanzania. Kwa pamoja, tutengeneze njia ambayo inasimamia haki, kuhifadhi mazingira yetu na kukuza mustakabali endelevu kwa wote,” alisema.
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Mafunzo PAMS Foundation, Bw. Samson Kasala akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa PAMS Foundation, Bw. Krissie Clark kwenye ufunguzi wa kikao kazi hicho.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji na Mafunzo, Bw. Samson Kasala, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa PAMS Foundation, Bw. Krissie Clark alisema kuwa PAMS Foundation pamoja na IJA wameandaa warsha tano katika kipindi cha miaka iliyopita juu ya kushughulikia kesi za makosa ya wanyamapori na misitu kwa wadau wote wa haki.

“Warsha hizi zilileta pamoja jumla ya washiriki 827 kutoa nchi nzima, wakiwemo Majaji 38, Mahakimu 247, Mawakili wa Serikali 237 na Wapelelezi 205. Hii ni idadi kubwa ya washiriki na tunawashukuru sana Viongozi kwa kuwezesha mahudhurio yao katika warsha hizi muhimu,” alisema.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) katika picha ya pamoja. Wengine ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Uendeshaji na Mafunzo PAMS Foundation, Bw. Samson Kasala (wa pili kulia), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa Wanyamapori, Divisheni ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata U. Msoffe (wa kwanza kushoto). Picha chini ni meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa kikao kazi hicho.

Mkurugenzi Mtendaji alieleza pia kuwa wanaamini warsha hizo zimekuwa muhimu katika kukuza ujuzi mpya, kuchochea mijadala inayohitajika na kuwezesha uelewa wa pamoja kupitia vikao hivyo vya pamoja.
Kikao kazi hicho kimeandaliwa na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya PAMS Foundation inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na usalama wa wanyamapori.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news