Ushirikiano wa wadau waleta matokeo chanya Mahakama ya Wilaya ya Kibaha

NA EUNICE LUGIANA
Mhakama Pwani

HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai amewapongeza wadau wa haki jinai kwa kushirikiana na Mahakama hiyo na kuwezesha kumaliza mrundikano wa mashauri.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Mahakama ya Wilaya Kibaha (Kulia), Mhe. Emmael Lukumai (kushoto) na Wakili wa Serikali, Bi. Elizabeth Olomi wakiendesha Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika Juni 20, 2024 katika Mahakama hiyo.

Mhe. Lukumai ametoa pongezi hizo Juni, 20,2024 katika kikao cha kusukuma mashauri ya madai ambacho amekiongoza yeye Mwenyekiti.

“Kama tulivyokubaliana kuwa, ifikapo Aprili, 2024 mashauri yote yanayoonekana yanakaribia kwenye mlundikano yawe yameisha na kweli imekuwa hivyo tujipongeze wote kwa hatua hii maana azimio letu limetimia,” amesema Mhe. Lukumai.
Mwenyekiti wa Kikao Cha Kusukuma Mashauri ya Madai (Bench Bar), Mhe. Emmael Lukumai (kushoto) na Katibu, Bi. Rita Ntagazwa wakiongoza kikao hicho Juni 20, 2024.

Amewaomba upande wa Mashtaka na Polisi kukubaliana kuwa na maahirisho mafupi na kuongeza kuwa, sasa hivi tuko katika mtandao hivyo hata wito kwa mashahidi (summons) zitumwe tu kwa njia ya mtandao.

Kadhalika Mfawidhi huyo, amewataka Mawakili wa Kujitegemea kuangalia shajara zao ili kuepuka kuchelewesha mashauri ambapo amesema kwamba, mashauri mengi yenye uwakilishi wa Mawakili mara nyingi yamekuwa yakichelewa kutokana na udhuru wa Mawakili kwa kutokupanga vizuri shajara zao.
Mwakilishi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Rita Ntagazwa (kushoto) akipokea malalamiko dhidi ya Mawakili wa Kujitegemea. Kulia ni Wakili wa Serikali, Bi. Gladness Mchami akisikiliza na kufuatilia mjadala.

Naye, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mhe. Felister Ng’hwelo amesema mashauri mengi ya Mawakili huwa na ucheleweshaji, ambapo amebainisha kuwa, wengi wao hawana sababu za msingi za kuahirisha mashauri hayo.

Akitoa mfano, Mhe. Ng’hwelo amesema kwamba, alikuwa na shauri moja lenye Wakili ambaye hakutokea mahakamani kwa mara mbili na alituma Mwakilishi naye hakuwa na maelekezo ya kuendelea na shauri hilo, kufuatia hali hiyo, alifuta shuri hilo kwa kuwa hakukuwa na sababu za msingi za ucheleweshaji. Hivyo, wamemuomba Mwakilishi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Pwani, Rita Ntagazwa awafikishie taarifa hiyo ili wafuate taratibu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Joseph Luoga akifuatilia yanayojiri katika kikao pamoja na Wadau.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Ntagazwa amesema Wakili anayetoa udhuru kuwa yuko Mahakama alete uthibitisho wa wito (summons) au ‘causelist’, lakini pia amewaomba Mahakimu pia kutokulazimisha tarehe ambayo Wakili anasema ana shauri mahali pengine na kusema kuwa, itasaidia kuondokana na usumbufu wa kutofika mahakamani wakati mashaidi wameshafika.

Naye Wakili wa Serikali, Dorice Kawonga amewaomba Ustawi wa Jamii kuongeza watu wanaoshughulikia masuala ya watoto maana katika Mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi Pwani mpaka sasa anayetegemewa katika masuala hayo ni mmoja pekee.
Wakili wa Serikali, Bi. Dorice Kawonga akiwasilisha hoja yake kuhusu Ustawi wa Jamii.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Joseph Luoga amewaomba wadau wa haki jinai kuipa thamani sawa Mahakama ya Mwanzo kama Mahakama zingine maana ndio Mahakama ya wananchi wa kawaida na inabeba asilimia 70 ya wananchi ukilinganisha na ngazi nyingine za juu na ndio maana Bunge likaona ni vema kufanya marekebisho ya Sheria na kuruhusu Mawakaili kuwawakilisha wateja wao katika Mahakama hiyo.

Mhe. Lukumai amewaomba Wadau hao kuendeleza ushirikiano uliopo pamoja na kutekeleza kwa pamoja yote waliokubaliana ili haki ipatikane kwa wakati.
Wawakilishi kutoka Ustawi wa Jamii, Misitu pamoja na Mahakimu wakiwa katika kikao hicho.

Katika kikao kilichopita maazimio yaliyofikiwa ambayo ni pamoja na kushauri zaidi wadaawa kufanya usuluhishi badala ya kusikiliza mashauri na kuwaelekeza Mawakili wa Kujitegemea kufuata utaratibu wa kisheria pindi wanapokuwa Mahakama za Mwanzo yote yametekelezwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news