PWANI-Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imeendelea kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa kamati mbalimbali za maafa katika ngazi ya wilaya na mikoa ili kuendelea kupunguza athari za maafa nchini.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia mawasilisho wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya kupunguza maafa kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani tarehe 24 Juni, 2024.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo ya siku tano kuanzia tarehe 24 hadi 29 Juni, 2024 yanayolenga juwajengea uwezo juu ya kupunguza maafa kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Luteni Kanali Selestine Masalamado amesema kuwa mafunzo haya ni muhimu ambapo yataweza kuongeza uelewa na ujuzi katika Shughuli za Usimamizi wa Maafa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Luteni Kanali Selestine Masalamado akitoa neno la Ukaribisho wakati wa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo juu ya Kupunguza Maafa kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani tarehe 24 Juni, 2024.
"Niwapongeze kuwa sehemu ya mafunzo haya kwa sababu Uzoefu unaonesha kuwa kuchukua hatua za mapema za kuzuia na kupunguza madhara zimekuwa na gharama nafuu kuliko kusubiri ili kuchuku hatua baada ya maafa kutokea ambapo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi hivyo basi kupitia mada mbalimbali zitakazo wasilishwa hapa ninaamini tutaongeza Uelewa na ujuzi wa Shughuli hizi za Maafa,"alisema Luteni Kanali Masalamado.
Mshauri Mwandamizi kutoka Timu ya kukabiliana na Maafa Mkoa wa Dar es Salaam (DarMAERT), Dkt. Christopher Mnzava akitoa mafunzo kuhusu Uelewa wa dhana za msingi za kupunguza adhari za Maafa (DRR) na Maudhui 24 Juni, 2024 katika Wilaya ya Rufiji.
Katika hatua nyingine amewashukuru wadau wa maendeleo kutoka UNDP pamoja na ngazi ya Taifa Kwa kujitoa na kuwezesha mafunzo ya mara kwa mara ya kujenga uwezo kwa wasimamizi wa maafa.
Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bw. Yona Benjamin akitoa wasilisho kuhusu Mzingo wa Menejimenti ya Maafa, Miundo ya Kitaifa ya Utekelezaji, Mifumo ya Sera, Tathmini na Uratibu wa kudhibiti Maafa tarehe 24 Juni, 2024.
"Nitumie fursa hii kuwashukuru wenzetu wadau wa maendeleo kutoka UNDP kwa kutuwezesha mafunzo haya lakini pia niwashukuru Ngazi ya Taifa kwa kujitoa na ninaamini washiriki watapata mafunzo sahihi na kwakuwa maafa ni jukumu letu sote kila mmoja ashiriki kuchukua hatua katika eneo lake ili kuokoa na kulinda maisha, mali na mazingira,"alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele akizungumza wakati akifungua Mafunzo ya Kuwajengea uwezo juu ya Kupunguza Maafa kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani tarehe 24 Juni, 2024.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amesema mafunzo haya ni muhimu kwa watendaji kazi ambapo kwa kuzingatia sheria ya usimamizi wa Maafa itatusaidia kuongeza nguvu katika kukabili maafa kabla hayajajitokeza.
"Nafurahi mafunzo haya yamekuja kwetu maana miezi iliyopita tulipata Maafa ya mafuriko hivyo kupitia mafunzo haya naamini hii ni fursa nzuri ya kujifunza namna ya kukabili jambo hili,"alisema Mhe. Meja Gowele.