VIDEO:Kiwanda cha kuongeza thamani Graphite mbioni kujengwa Mtwara

DODOMA-Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa, Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Limited (VGT) ipo katika majadiliano ya mwisho na wanunuzi wa Madini ya Kinywe (Graphite) ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya madini hayo Wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara.
Ameyasema hayo leo Juni 07, 2024, Bungeni, Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ndanda Mhe. Cecil Mwambe aliyetaka kujua kuhusu mpango wa Serikali kuhakikisha uchimbaji wa madini ya Kinywe unatekelezwa katika Kata ya Chiwata, Wilayani Masasi.

Akijibu, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Wizara ya Madini ilitoa leseni mbili za Uchimbaji wa Kati zenye namba ML 591/2018 na ML 592/2018 kwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Public Limited ili kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya kinywe katika mradi wa Mbunyu, Ndanda.

Amesema, hata hivyo, uchimbaji huo haujaanza tangu leseni hizo kutolewa kutokana na kuchelewa kwa makubaliano kati ya VGT na wanunuzi wa madini hayo.

Naibu Waziri Kiruswa ameongeza kuwa, kwa sasa, mwekezaji amesaini mkataba na Kampuni ya Property Matrix Limited (PML) kwa ajili ya kufanya tathmini ya ulipaji fidia kwa wananchi waliopo kwenye eneo la mradi. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha fidia stahiki inatolewa kwa wakazi ambao watapitiwa na mradi huo.

“Aidha, Kampuni ya Volt Graphite Tanzania ipo katika majadiliano ya mwisho na wanunuzi wa madini ya kinywe ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya madini hayo,” amesema Dkt. Kiruswa.

Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, Mradi wa Mbunyu utakapoanza kutekelezwa unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wakazi wa Kata ya Chiwata na Jimbo la Ndanda kwa ujumla kupitia ajira, maendeleo ya kiuchumi, na kuimarisha miundombinu katika eneo hilo.

Ametoa wito kwa wanaozunguka mradi huo kuchangamkia fursa za kutoa huduma katika mradi huo pindi shughuli za uchimbaji zitakapoanza baada ya kukamilika kwa majadiliano na taratibu zote zinazohitajika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news