NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu),Dkt. Charles Msonde amesema walimu nchini wanamsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jukumu la kuwapatia ujuzi watoto wa shule za msingi na sekondari, ili hapo baadae waweze kuendesha maisha yao na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Msonde amesema hayo, wakati wa kikao kazi chake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na maafisa hao.
“Ninyi walimu ni wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, kwani hayupo mtanzania yeyote tofauti na mwalimu aliyepewa dhamana ya kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata ujuzi shuleni,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chao na Naibu Katibu Mkuu huyo.
Dkt. Msonde amefafanua kuwa, mwalimu ndiye aliyepewa dhamana ya kuhakikisha watoto wa darasa la kwanza wanajua kusoma na kuandika na watoto wa sekondari wanajua kiingereza ambacho ni lugha rasmi ya kufundishia.
Dkt. Msonde amewataka walimu nchini kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuleta mapinduzi ya elimu ili taifa lizalishe wataalam wa fani mbalimbali watakao liwezesha taifa kupiga hatua katika maendeleo.
“Ninatambua jukumu la kuleta mabadiliko chanya katika elimu si dogo, lakini nina amini kuwa walimu wa uvinza na walio katika maeneo mengine mtaweza kutekeleza jukumu hili kwa kutoa mchango utakao boresha elimu kama ilivyokusudiwa na Mheshimiwa Rais,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma Bi. Paulina Ndigeza amesema walimu wa uvinza na mkoa mzima ni waumini wa mabadiliko, hivyo watageuza changamoto zinazowakabili kuwa fursa za kuboresha elimu mkoani Kigoma.
Dkt. Msonde amehitimisha ziara yake ya kuhimiza uwajibikaji katika halmashsauri zote zilizopo mkoani Kigoma kwa kufanya kikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.