Walimu zingatieni uwezo wa wanafunzi mnapofundisha-Dkt.Msonde

NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu), Dkt. Charles Msonde amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari nchini kuzingatia uwezo wa wanafunzi wanapofundisha ili wanafunzi wapate elimu na ujuzi stahiki kama ilivyoanishwa kwenye mtaala mpya ulioanza kutekelezwa Januari 2024 kwa madarasa ya awali, msingi na sekondari.
Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa walimu akiwa katika shule ya Sekondari Usinge, wakati wa kikao kazi chake na baadhi ya Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.
“Mwalimu unapofundisha watoto darasa lolote hata kama umendaa mpango kazi, maazimio ya kazi na andalio la somo unapaswa kukumbuka kuwa ufundishaji wako utategemea uwezo wa watoto unaowafundisha,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amehimiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inataka mabadiliko ya vitendo kwa walimu, hivyo walimu wanapaswa kuamua kuachana na mazoea ili wafundishe watoto kwa ufanisi na kwa kuzingatia weledi.
Dkt. Msonde ameongeza kuwa, walimu ni lazima waamini kwamba kuna changamoto katika ufundishaji wao kwasababu haiwezekani mwalimu ufundishe watoto kiingereza mwaka mzima alafu wasijue kusoma, kuandika na kuzungumza hali inayopelekea kupata ufaulu usioridhisha katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.

“Walimu tukiamini kwamba tuna changamoto, tuchukue hatua ya kubadilisha mitazamo yetu na kufanya tofauti na mazoea ambayo yametukwamisha na kutufikisha hapa tulipo,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Tabora Bw. Juma Kaponda amesema, anatamani walimu wa Kaliua na maeneo mengine nchini watekeleze hata robo ya maelekezo aliyoyatoa Dkt. Msonde ambayo yamelenga kuleta mapinduzi katika sekta ya elimu kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Msonde ameanza ziara ya kuhimiza uwajibikaji kwa walimu mkoani Tabora kwa kufanya vikao kazi viwili na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news