MOROGORO-Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amewashauri waandishi wa Habari za Biashara na Uchumi kuendelea kuwafikishia wananchi taarifa sahihi zinazohusu Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).


Amefafanua kuwa wameanza na waandishi hao wa habari za biashara kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na hasa wanaondika habari za BRELA lakini mikakati yao ni kwamba mafunzo hayo yatatolewa kwa waandishi wa Mikoa yote na lengo ni kuhakikisha wanaendelea kuwajengea uwezo wadau muhimu wakiwemo waandishi wa habari.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa amesema sababu za mafunzo ni moja ya utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kuhakikisha inatoa elimu kwa umma na wadau mbalimbali.
“Tumeshuhudia baadhi ya habari ambazo zinaripotiwa lakini zina makosa mengi. Namna ya kupunguza makosa hayo ya kiuandishi wa habari za Kibiashara ni kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wanahabari ili kuondoa makosa hayo huku akisisitiza kwamba kupitia Wakurugenzi wa Wakala huo watatoa elimu ya kutosha katika mafunzo hayo na waandishi wa habari wasisite kuuliza kwa lengo la kujifunza zaidi,”amesema Nyaisa.

Pia amesema kuanzia sasa wataanza kutoa tuzo Maalum kwa waandishi wa habari za biashara ambao watakuwa wakiandika makala zenye matokeo chanya kwa jamii lakini makala ambazo zitakuwa zimejitosheleza.