ARUSHA-Wataalam wa sekta ya afya kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika kikao cha maandalizi ya Mkutano wa Saba (7) wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya utakaofanyika kesho tarehe 14 Juni, 2024 na kutanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu.
Mkutano huu wa wataalamu pamoja na masuala mengine utapitia na kujadili pendekezo la Tanzania la kuanzisha vituo viwili vya umahiri ambavyo ni: Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka ameeleza kuwa kupitia mkutano huu wajumbe watachangia na kushauri juu ya umuhimu wa vituo hivyo viwili vya umahiri ambavyo vinachangia utoaji wa huduma za kibingwa za afya pamoja na mafunzo katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naye Mwenyekiti wa mkutano wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Dut katika hotuba yake ya ufunguzi ameeleza kuwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 kumeleta somo katika ukanda wa Afrika Mashariki hususan katika suala la kujijengea uwezo wa kujitegemea katika masuala ya huduma za afya, uanzishaji wa programu saidizi na uimarishwaji wa miundombinu katika sekta hiyo.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano Ngazi ya Wataalam umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka ambaye ameambatana na Wataalamu Waandamizi kutoka sekta ya Afya na Elimu.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Mhandisi amesisitiza umuhimu wa mkutano huo, akibainisha kuwa andiko dhana ya kuanzisha vituo vya umahiri vilivyopendekezwa na Tanzania vitaleta mabadiliko muhimu katika mifumo ya afya, huduma za kibingwa, mafunzo, na kujengea uwezo.
Pia, amewahimiza wajumbe kujadili na kushiriki katika mijadala ya wazi na yenye kujenga ili kuboresha afya kwa ustawi wa watu wa EAC, huku akitoa shukrani kwa wadau wote walioshiriki katika kuandaa maandiko haya ya dhana.
Mwenyekiti wa Mkutano wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Rut (wa pili kushoto) akifungua Mkutano Ngazi ya Wataalamu kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Saba (7) wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya utakaofanyika tarehe 14 Juni, 2024 jijini Arusha. Kulia kwake ni: Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka, Mkuu wa Idara ya Afya kutoka kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Eric Nzeyimana na kushoto ni Mnukuu (Rapportuer) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Dkt. Dieumerci Kaseso.
Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka (kati) akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano Ngazi ya Wataalam unaofanyika tarehe 13 Juni, 2024 jijini Arusha.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akitoa neno la ufunguzi katika Mkutano Ngazi wa Wataalam unaofanyika jijini Arusha tarehe 13 Juni, 2024.
Ujumbe kutoka Tanzania.
Ujumbe kutoka Uganda.
Ujumbe kutoka Tanzania.
Sehemu nyingine ya Ujumbe kutoka Tanzania.
Picha ya pamoja.