DAR-Athari za maendeleo na mabadiliko ya teknolojia zimetajwa kuathiri mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji katika elimu hususani vyuo vikuu ambavyo ndizo taasisi zinazotarajiwa kuzalisha nguvu kazi ya taifa. Kwa minajili hiyo, maofisa wa uthibiti ubora, waratibu na watendaji wamehimizwa kuliangalia upya swala hili na kurekebisha mitaala ili kuendana na mabadiliko hayo ya teknolojia na maisha.
Akifungua Mkutano wa Saba wa Jukwaa la Wathibiti Ubora wa Vyuo Vikuu Tanzania (TUQAF), Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda, amewahimiza maofisa uthibiti ubora, watendaji na waratibu kusimamia na kufikiri namna ya kubadili mitaala ya elimu na njia za ufundishaji ili kuendana na maendeleo ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.
“Kaulimbiu ya kongamano imeendana na wakati huu ambapo kuna mabadiliko ya teknolojia katika elimu, lazima tuanze kufikiria njia tofauti itakayotusaidia kutoa masomo yanayoendana na maisha halisi.
"Pia tufanyie tafiti na kufuatilia mwenendo wa teknolojia, ilivyo sasa sivyo ilivyokuwa miaka 40 iliyopita. Tunapaswa kufanyia kazi mabadiliko katika elimu, ili anachofundishwa mwanafunzi shuleni kitumike nyumbani na anachofanya nyumbani kitumike shuleni,” amesema Prof. Bisanda.
Naye Rais wa Jukwaa la TUQAF, Prof. Justin Urassa, amesisitiza umuhimu wa mkutano wa jukwaa hilo kujadili yatakayokwenda kuboresha na kuwa chachu ya mapendekezo ya namna ya kuhakikisha ubora wa elimu inayotolewa unaenda kwa mujibu wa huduma katika vyuo vikuu.
Akizungumza katika mkutano huo Profesa Justin Urassa, amevipongeza vyuo vikuu ambavyo tayari vimeshakuwa na idara za uthibiti ubora, ambazo kimsingi ndizo zinajishughulisha na shughuli zote za kuthibiti ubora katika taasisi za elimu ya juu Tanzania.
“Navipongeza vyuo vikuu ambavyo tayari vimeshakuwa na idara za uthibiti ubora, idara hizo ndizo zinajishughulisha na shughuli zote za kuthibiti ubora katika mitaala na huduma zinazotolewa vyuoni. Ili kuwapata wahitimu wenye ujuzi, lazima idara hizi za uthibiti ubora zihakikishe huduma bora zinatolewa kwa wanafunzi,” amesema Prof. Urassa.
Akitoa neno la shukrani, Dkt. Jeniffer Sesabo ambaye pia ni mmoja wa waasisi wa jukwaa hilo, amewakumbusha washiriki kuwa wameandaliwa mkutano huo nje ya maeneo yao ya kazi ili kuwapa nafasi ya kufikiri upya njia mbadala ya kubuni mitaala mipya inayoendana na hali ya sasa.
“Tunapaswa kuvishauri vyuo vikuu njia bora za kutoa mitaala mipya huku pia tukifanyia kazi ujuzi na maarifa husika katika soko la ajira. Elimu inayotolewa inapaswa kuwa ya ubunifu,” amesema Dkt. Sesabo.
Jukwaa la uthibiti ubora wa vyuo vikuu linaundwa na wathibiti ubora kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Jukwaa hilo limefanya mkutano wake wa saba kwa siku mbili kuanzia Mei 21 na Mei 22, 2024, Makao Makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo masuala mbalimbali yahusuyo uthibiti ubora yamejadiliwa ikiwamo mijadala ya namna ya kuthibiti ubora na kuzingatia mitaala yenye misingi ya umahiri.
Pia, ujuzi na elimu jumuishi. Pia majadiliano yalijikita katika kutengeneza mitaala ya elimu mtandao na majukumu ya wathibiti ubora katika elimu mtandao hasa ngazi za vyuo vikuu.
Mbali na kufanya mikutano ya kila mwaka TUQAF ni tawi la mtandao wa uthibiti ubora wa Afrika Mashariki (East African Quality Assurance Network).
Kwa Pamoja TUQAF na EAQAN hutoa fursa kwa wathibiti ubora wa Afrika mashariki kuwasilisha tafiti zao zenye lengo la kupeana uzoefu na ujuzi katika kuthibiti ubora katika taasisi za elimu ya juu na hatimae taifa kwa ujumla.