Watumishi Tume ya Madini watakiwa kutenga muda wa mazoezi, waonesha vipaji Tanga

TANGA-Tume ya Madini imewataka watumishi wake nchini kutumia muda mwingi kufanya kazi huku wakitenga muda wa kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbali mbali ili kuimarisha afya ya mwili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumza leo Juni 14, 2024 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Ramadhan Lwamo amesema siku zote afya ndio kazi , afya mgogoro hakuna kazi.
Mhandisi Lwamo ameyasema hayo akifunga Bonanza la Wakurugenzi, Mameneja kutoka Tume ya Madini Makao Makuu Dodoma na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa lililofanyika kwenye uwanja wa Donge TFF jijini Tanga.

"Michezo ni furaha, inaimarisha mahusiano na kuboresha afya zetu watumishi, baada ya bonaza ‘reflection’ yake tunaiona kwenye matokeo ya kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali,”amesema Lwamo.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Tume CPA. William Mtinya akizungumza amesema, Tume imeweka utaratibu wa kuhamasisha watumishi wake kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbali mbali ili kuwaweka vyema kiafya na kuwa imara katika utendaji kazi wao.

Amesema, pia tume inatekeleza maagizo ya Serikali kwamba kila Taasisi idumishe michezo ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakisumbua jamii na kwamba bonanza hilo pia huleta mshikamano wa wafanyakazi na kubadilishana mawazo.

“Tumekutana kujadili mikakati ya kukusanya maduhuli ya Serikali, kuimarisha afya zetu na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kimsingi mchezo ulikuwa upande wetu na tumefanikiwa kuwafunga magoli mawili bila,”amesema CPA Mtinya.
Naye Afisa Madini Mkazi wa Kahama, Mhandisi Joseph Kumburu akizungumzia matokeo ya kufungwa mabao mawili kwa bila amesema kuwa wamekubali matokeo, walizidiwa na mchezo.

“Kipindi cha kwanza wenzetu wa Makao Makuu wamecheza vizuri kipindi cha pili tulikuwa na majeruhi, mpira ulikuwa mzuri bahati haikuwa ya kwetu,”amesema Mhandisi Kumburu.

Katika Bonanza hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Donge TFF jijini Tanga, Timu ya soka ya Tume ya Madini kutoka Makao Makuu Dodoma iliibugiza RMO’s mabao 2-0 na kutwaa Kombe.

Katika bonanza hilo vikombe na medani zimetolewa kwa washindi ikiwa ni pamoja na mfungaji bora katika mchezo wa mpira wa miguu Azihar Kashakara kutoka Tume Makao Makuu, mlinda mlango bora CPA Wiliam Mtinya kutoka Tume Makao Makuu na mchezaji bora Mhandisi Sabai Nyansiri kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi- Singida.
Mbali na mpira wa miguu pia bonanza hilo limehusisha michezo ya kuvuta kamba, kukimbia mita 100 na kufukuza kuku ambapo washindi wamekabidhiwa medani mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news