Waziri Dkt.Nchemba ataja sababu za kuanzishwa taasisi hizi

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema,hadi Aprili 2024, wizara imefanikiwa kuanzisha Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

Sambamba na Ofisi ya Akaunti ya Changamoto za Milenia ikiwemo kuzindua na kuwezesha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi kuanza kutoa huduma.
Ameyasema hayo leo Juni 4,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

"Katika mwaka 2023/24, wizara iliendelea kufanya mapitio na kuboresha miundo ya kitaasisi ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake."

Amesema, lengo la kuanzisha taasisi hizo ni kuimarisha na kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa mipango ya Serikali.

Vile vile, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini hususani kuondoa au kupunguza vikwazo vya kibiashara na malalamiko ya walipakodi.

Pia, amesema wizara imefanikiwa kukamilisha mchakato wa kuchagua eneo la ushirikiano na Shirika la Changamoto za Milenia la Marekani- MCC.

"Pamoja na mambo mengine, msaada utakaotolewa na shirika hilo utatumika kutekeleza programu za maendeleo zinazolenga kupunguza au kuondoa vikwazo vya kibiashara."

Mbali na hayo, Waziri Dkt.Nchemba amesema, hadi Aprili 2024, wizara yake imetoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu ili kuziwezesha mamlaka za Serikali kuandaa miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa utaratibu wa ubia.

Amesema, ushauri na mafunzo ya kitaalamu yametolewa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika kuandaa nyaraka za mradi wa barabara ya haraka kutoka Kibaha hadi Morogoro (kilomita 205).

Waziri Dkt.Nchemba amesema, hatua za ununuzi wa mbia zinaendelea kwa sehemu ya Kibaha-Mlandizi-Chalinze (kilomita 78.9) na Wakala wa Mabasi Yaendayokasi kuhusu ununuzi wa mbia wa uendeshaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam.

Aidha, amesema mashauriano yanaendelea kuhusu upanuzi na ujenzi wa barabara ya haraka kati ya Morogoro na Dodoma kwa utaratibu wa ubia.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Nchemba amesema, hadi Aprili 2024, jumla ya taasisi za umma 334 zimewezeshwa kuandaa, kuhuisha na kuweka kumbukumbu ya mali zenye thamani ya shilingi trilioni 13.66 katika mfumo wa GAMIS.

"Aidha, katika kipindi hicho, wizara imetoa vibali 123 vya kuondosha mali chakavu na kuwezesha minada 100 katika taasisi za umma ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.6 zilikusanywa katika minada hiyo."

Vilevile, amesema wizara imefanya uhakiki wa mali katika vituo 388 vya Serikali ambapo taarifa zimeandaliwa na mapendekezo kuwasilishwa kwa maafisa masuuli kwa hatua stahiki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news