Waziri Dkt.Nchemba ataja vigezo ujenzi wa Kituo cha Forodha

NA PETER HAULE

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amemshauri Mbunge wa Ngara, Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro kushirikiana na mamlaka husika ili kuangalia uwezekano wa ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma mkoani Kagera baada ya kujiridhisha pasipo shaka iwapo eneo hilo linafaa kwa ujenzi wa kituo hicho.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Ngara, Mhe. Ndaisaba George Ruhoro, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Wizara ya Fedha).

Mhe. Dkt. Nchemba alisema hayo bungeni, jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Mhe. Ndaisaba George Ruhoro, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma.

Alisema kuwa, endapo mamlaka husika zitajiridhisha pasipo shaka kuhusu eneo hilo kutokuwa na madhara kwa nchi kiuchumi, kijamii na kiusalama, Serikali itashauriwa kuyafanyia kazi maombi hayo.

“Kabla ya eneo au kituo kuteuliwa kuwa eneo la Forodha na kuweza kufunguliwa kama kituo cha forodha mahali popote nchini kuna taratibu za kisheria ambazo inabidi zifuatwe,”amesema Dkt.Nchemba.

Alieleza utaratibu huo kuwa ni pamoja na kutangazwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya Mwaka 2004, Kifungu Namba 11.

Dkt. Nchemba alisema kuwa baada ya Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa kupokea maombi ya kuteua eneo husika kuwa eneo la forodha kutoka kwa Waziri mwenye dhamana, huwasilisha pendekezo la kuteua kituo husika kwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news