Waziri Mkuu ataka hatua zichukuliwe kuondoa udumavu

*Ataka mikoa inayoongoza ianze urutubishaji wa chakula kuanzia ngazi za vijiji

DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Mikoa yenye viwango vikubwa vya upungufu wa damu na udumavu ianze kutekeleza mpango wa urutubishaji wa chakula kuanzia ngazi ya vijiji ili baada ya miaka mitano kuanzia sasa zaidi ya nusu ya Watanzania wawe wanatumia chakula kilichorutubishwa.“Hatua hii itachochea kasi ya kupungua kwa vifo vya akina mama wanaojifungua pamoja na watoto wachanga kutokana matatizo yanayohusiana na upungufu wa damu mwilini, na kupungua kwa kinga mwili. Vilevile, itapunguza matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa watoto.”
Pia, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na wadau wote wa lishe washirikiane katika kuandaa mkakati mahsusi wa kuelimisha umma na kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana wa umuhimu wa virutubishi vinavyochanganywa kwenye chakula katika kukabiliana na changamoto za lishe duni.

Ametoa maagizo hayo leo Jumamosi, Juni 15, 2024 wakati wa Uzinduzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Virutubishi na Tovuti ya Wasindikaji Chakula Tanzania kilichipo Mikocheni jijini Dar es Salaam. Amesema ili kulinda afya za walaji, wasindikaji wote wazingatie namna ya kutunza virutubishi na vinyunyizi vya virutubishi ili visiharibike. Kiwanda hicho ni cha kwanza kwa Afrika Mashariki na cha pili kwa Afrika.
Waziri Mkuu amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya mkakati mpya wa juhudi za Serikali na washirika wake katika kuwezesha usindikaji bora zaidi na uwekaji virutubishi kukidhi mahitaji ya mwili.

"Urutubishaji huo utaendelea kupunguza viwango vya vifo vya akina mama wanaojifungua pamoja na vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na matatizo yanayohusiana na upungufu wa damu mwilini.”

Amesema urutubushaji huo utaimarisha afya ya watoto wa kike walio katika rika balehe kwa kuwapunguzia changamoto ya upungufu wa damu, vilevile utasaidia kuimarisha afya za watoto kwa kukabiliana na tatizo la kupungua kinga mwilini ambalo ni chanzo cha watoto kuugua mara kwa mara, lakini pia kupunguza matatizo ya vichwa vikubwa, mdomo sungura na mgongo wazi kwa watoto.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa tovuti ambayo ni mahsusi kwa ajili ya mtandao wa wasindikaji wote wa chakula hasa unga na mafuta ya kula, Waziri Mkuu amesema mtandao huo una manufaa makubwa kwani pamoja na mambo mengine, unakusudiwa kutumika katika kutoa elimu na kuongeza ujuzi kutoka kwa wasindikaji wakubwa waliobobea kwenye teknolojia ya usindikaji chakula hapa nchini na kwingineko duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news