DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Madini iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kutafuta teknolojia mbalimbali za uongezaji thamani madini.
.jpg)
Ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Juni 27, 2024 wakati alipofunga wiki ya madini iliyoambatana na Kongamano la Wachimbaji Madini, Mkutano Mkuu wa FEMATA pamoja na Maonesho ya Madini na Vifaa vya Uchimbaji iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa Wafanyabiashara, Taasisi za Elimu, Taasisi za Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Madini kuendelea kuweka mikakati ya kuwezesha uwekezaji wa ndani wa teknolojia mbalimbali nchini zitakazowezesha upatikanaji wa malighafi zinazohitajika na migodi na shughuli nyingine za madini.
.jpg)

"Kwa kujifungia ndani peke yetu hatutapata suluhisho la changamoto tulizonazo bali tutachelewesha maendeleo yetu."
.jpg)
“Katika hili nitoe wito kwa taasisi za fedha nchini kukaa na FEMATA, wapeni miongozo na elimu ya mitaji ili waweze kuitumia katika kuzipa thamani kazi zao ili ziwe na tija.”
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa nguvu sekta ya madini ili iendelee kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 hadi kufikia shilingi bilioni 231.
“Mipango yetu ni kuendelea kufanya tafiti za kina ili kubaini sehemu yalipo madini, pia tumepanga kununua helkopta ya kisasa ya itakayobaini kilichopo hadi urefu wa kilomita moja chini ya ardhi pamoja na kujenga maabara kubwa ya kisasa katika sekta ya madini.”
Pia Mheshimiwa Mavunde amesema Wizara inaendelea kutekeleza mpango wa kufuta leseni na maombi kwa wawekezaji waliochukua maeneo makubwa ya uchimbaji madini lakini hawayaendelezi na kuwapatia Watanzania wenye nia ya kuchimba ili wanufaike na rasilimali hiyo muhimu.

Aidha, amesema kuwa katika mwaka 2024-2025 FEMATA imepanga kuendelea kuwaomgezea ujuzi na maarifa wachimbaji wadogo wengi zaidi pamoja na kuwaunganisha na Serikali ili kusaidia kuongeza vipato vyao na Taifa kwa ujumla.
“Pia tumeandaa vitambulisho ili tuweze kutambua kila mchimbaji alipo na anafanya nini.”