Waziri Mkuu awapa kongole watumishi wa umma

DODOMA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewapongeza watumishi wa umma nchini kwa kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa kufanya kazi kwa bidii.
Pongezi hizo amezitoa leo Juni 23, 2024 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

"Kwanza naipongeza wizara kwa maadhimisho haya ya Wiki ya Utumishi wa Umma, lakini vilevile ninawapongeza watumishi wa umma kwa uwajibikaji wenu uliotukuka wa kuwatumikia Watanzania.

"Matokeo chanya yanaonekana na yanaedelea kushuhudiwa na Watanzania, Mheshimiwa Rais amesema, kazi iendelee na hatawaangusha kamwe."

Pia, Waziri Mkuu amewapongeza wataalamu wazawa waliohusika kuandaa mifumo ambayo ameizindua leo.

Mifumo iliyozinduliwa ni Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-WATUMISHI), Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi (PEPMIS kwa watumishi wa umma na PIPMIS kwa taasisi za umma).

Pia, Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR Assessment) na Mfumo wa e-Mrejesho.

Amesema, maadhimisho hayo ya kila mwaka ndani ya mwezi Juni yanalenga kuhimiza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika Utumishi wa Umma.

Katika maadhimisho hayo, Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) lilikuwa miongoni mwa taasisi za umma ambazo zilishiriki tangu Juni 16 hadi leo.
Ushiriki wa NHC katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, uliwapa fursa wananchi na wadau mbalimbali kupata huduma na kufahamishwa kuhusu miradi ya shirika hilo hapa nchini.

Wadau hao pia, walipata fursa ya kuifahamu baadhi ya miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na NHC kwa ajili ya makazi na biashara katika maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa miradi hiyo ni Morocco Square, Kawe 711 na Samia Housing Scheme uliopo Tanganyika Packers Kawe jijini Dar es Salaam.
Mingine ni Iyumbu, Medeli na mji wa Serikali ambapo NHC inajenga majengo mbalimbali ya wizara za Serikali.

Maadhimisho na Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kitaifa yameratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo kaulimbiu ya nwaka huu ni “Kuwezesha kwa Utumishi wa Umma uliojikita kwa Umma wa Afrika ya Karne ya 21 iliyojumuishi na inayostawi; Ni Safari ya Mafunzo na Mabadiliko ya Kiteknolojia”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news