DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua vitabu vya historia ya Bunge ambavyo vitasaidia kuhamasisha tafiti na kujua zaidi kuhusu mchango wa Bunge katika maendeleo ya jamii nchini.
Amesema kuwa, vitabu hivyo pia vitakuwa kielelezo cha mafanikio na changamoto ilizopitia Bunge la Tanzania katika kudumisha demokrasia na utawala wa sheria.
“Historia yetu ni sehemu ya mchango wetu kwa jumuiya ya kimataifa katika kukuza amani, utulivu na maendeleo.”
Amesema hayo leo Jumatano, Juni 26, 2024 wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vya historia ya bunge katika ukumbi wa Pius Msekwa, Jijini Dodoma.Vitabu vilivyozinduliwa ni Kitabu cha Historia ya Bunge kutoka 1926-2024 na Wabunge wa Tanzania na nafasi zao kuanzia mwaka 1965-2023.
“Kumbukumbu za historia ya Bunge zinaweza kuchochea utafiti wa kitaaluma na maendeleo ya nadharia za kisiasa na utawala. Watafiti wanaweza kutumia taarifa hizi kujenga ufahamu mpya na kupendekeza mifumo bora ya kisiasa.”
Kwa upande wake Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amepongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa sehemu ya maono ya bunge ikiwemo kuridhia kulikabidhi bunge maeneo yote yanayozunguka jengo la bunge.