DODOMA-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuendelea kushirikiana na Vyuo vya Elimu ya Juu nchini katika mchakato wa kufanya maboresho ya mitaala ili iendane na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mitaala Mipya ya ElimuMsingi.

Ameongeza kuwa majadiliano kati ya Tume hiyo na Vyuo Vikuu ni muhimu pamoja na kwamba TCU inaweza kutoa maelekezo lakini ni muhimu yafanyike kupitia majadiliano ili kuwa na ushirikishwaji wa wadau wa elimu ya juu.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa katika kutekeleza mageuzi ya elimu katika ngazi ya chini, vyuo vikuu vinapaswa kujipanga katika kuandaa walimu wanaokwenda kufundisha katika shule za Sekondari, hivyo ni lazima kuangalia nini sera inahitaji.
Waziri huyo amesema pia katika sera na mitaala iliyoboreshwa kuna masomo mapya ambayo yanahitaji walimu akitolea mfano somo la ujasiriamali ambalo halina walimu wa kutosha na kupelekea utekelezaji wa Sera mpya katika elimu ya Sekondari kuanza na Mkondo wa Amali pekee.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof. Charles Kihampa amesema kuwa kikao hicho kitajadili juu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mitaala mipya ya elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu na namna Vyuo Vikuu vitakavyoboresha Mitaala ili kuendana na mabadiliko haya