Wizara ya Fedha yashauriwa kufikisha Elimu ya Fedha kwa wananchi wote

NA JOSEPHINE MAJULA

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bi. Grace Quintine, ameishauri Wizara ya Fedha kuhakikisha Watanzania wote nchini wanapatiwa elimu ya fedha ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha na waweze kufanya maamuzi sahihi katika matumizi sahihi ya vipato vyao.
Mkazi wa Wilaya ya Urambo, Bi. Amina Kimenya, akisoma kipeperushi chenye taarifa za usimamizi wa fedha binafsi ambayo ni moja ya mada ambazo zinafundishwa na Timu ya Watalaamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo wilayani humo kutoa elimu ya fedha katika mada mbalimbali ikiwemo kuweka akiba, uwekezaji na mikopo mkoani Tabora.

Bi. Quintine ametoa ushauri huo alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika wilayani Urambo mkoani Tabora, kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi ili waweze kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Fedha na kujikomboa kiuchumi.

“Naamini Wananchi wote wakipatiwa elimu hii muhimu ya masuala ya fedha wataweza kuwa na nidhamu ya matumizi lakini pia watakuwa na uelewa wa wapi wakawekeze fedha zao ili kuongeza mitaji katika biashara zao na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,”alisema Bi. Quintine.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bi. Grace Quintine, akizungumza na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika ofisini kwake kujitambulisha na kuelezea njia watakazo tumia kufikisha elimu ya huduma ndogo za fedha katika Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bw. Sabhi Makongo, alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali ya masuala ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali ikiwemo watumishi, wanavikundi vya kinamama na jamii katika ngazi ya familia.

“Elimu ya fedha inahitajika sana kwa wananchi wa makundi mbalimbali hivyo sisi kama Halmashauri tutaendelea kutoa elimu hii mara kwa mara kwa wananchi wetu na kuwahamasisha kusajili vikundi vyao ili viweze kutambulika rasmi endapo fursa za mikopo zitatokea waweze kupata na kuongeza mitaji yao,” alisema Bw. Makongo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bi. Grace Quintine, akipokea kitabu chenye mada mbalimbali ikiwemo uwekezaji, akiba na mikopo zitakachotumika kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya hiyo kutoka kwa Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi.

Naye mkazi wa Wilaya ya Urambo Bi. Chiku Rajabu, alisema kupitia mafunzo aliyoyapata yamempa uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwa ni pamoja na kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia uwekezaji.
Mkazi wa Wilaya ya Urambo, Bi, Joyce Nyamilibo, akiuliza swali kuhusu uwekezaji kwa Timu ya Watalaamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo wilayani humo kutoa elimu ya fedha katika mada mbalimbali ikiwemo kuweka akiba, uwekezaji na mikopo mkoani Tabora.

“Naishukuru sana Serikali kuona umuhimu wa elimu hii kutufikia sisi wana Urambo, hakika elimu niliyoipata itanisaidia kupanga mipango sahihi katika matumizi ya fedha zangu,” alisema Bi. Rajabu.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Urambo, wakionesha fulana zenye kauli mbiu “Elimu ya Fedha Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi” walizopewa baada ya kujibu maswali wakati wa semina iliyotolewa na Wizara ya Fedha ambayo ipo wilayani humo kutoa elimu ya fedha katika mada mbalimbali ikiwemo kuweka akiba, uwekezaji na mikopo mkoani Tabora.

Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, alisema wapo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha.

“Katika utoaji elimu tunaonesha filamu ambayo imebeba mada mbalimbali ikiwemo masuala ya kujiwekea akiba, mikopo, kujiandaa na kustaafu, uwekezaji na bima,"alisema Bi. Bulugu.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Urambo wakiangalia filamu yenye mada mbalimbali kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha ambayo ilitumika na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kutoa elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Tabora.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Tabora).

Katika zoezi la kutoa elimu kwa Wananchi Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha imeambatana na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ikiwa ni Utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news