Wizara yafanya uhakiki wa mapendekezo ya fidia shilingi bilioni 37.79 kwa wananchi

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwingulu Lameck Nchemba amesema,hadi kufikia Aprili, 2024 wizara yake imefanya uhakiki wa mapendekezo ya fidia ya jumla ya shilingi bilioni 37.79 kwa wananchi walioridhia kuachia maeneo yao kupisha miradi ya maendeleo.

"Miongoni mwa majukumu ya Wizara ya Fedha ni ufuatiliaji na uhakiki wa mahitaji na matumizi ya fedha za umma.

"Hadi Aprili 2024, wizara imefanya uhakiki wa mapendekezo ya fidia ya jumla ya shilingi bilioni 37.79 kwa wananchi walioridhia kuachia maeneo yao kupisha miradi ya maendeleo;
Ameyasema hayo leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Nchemba amesema, wizara imefanya uhakiki wa madai ya fidia kwa wananchi wanaopisha maeneo yaliyotwaliwa na Serikali kwa ajili ya upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Pia, kwa upande wa viwanja vya ndege vya JNIA, KIA na Kigoma, ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maeneo ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika mikoa ya Pwani na Arusha.

"Vilevile, katika kipindi cha rejea, wizara imetoa nyaraka mbili za udhibiti wa bajeti za mafungu ya kisekta ili kukabiliana na msukumo wa mahitaji ya rasilimali fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususani mafuriko.

"Kadhalika, wizara imeandaa kitabu cha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24 Toleo la Wananchi, na kuandaa taarifa za utekelezaji wa bajeti ya Serikali kila robo mwaka na kuweka kwenye tovuti ya wizara ili kuongeza uwazi,"amebainisha Waziri Dkt.Nchemba.

Mbali na hayo, Waziri Dkt.Nchemba amesema, kwa mwaka 2023/24, wizara ilipanga kujenga uwezo wa wakaguzi wa ndani katika sekta ya umma ili kuendana na viwango vya kitaaluma vya Kimataifa (Certified Internal Auditor (CIA) na Certified Information System Auditor (CISA).

Aidha, kujenga uwezo kwa wakaguzi wa ndani katika taasisi za umma 13 kuhusu matumizi ya mfumo wa ukaguzi-Government Internal Audit Management Information System (GIA MIS), kujenga uwezo wa wakaguzi wa ndani katika maeneo ya ukaguzi wa taarifa za fedha na mchakato wa ukaguzi unaozingatia vihatarishi.

Kujenga uwezo wa maafisa masuuli na wenyeviti wa kamati za ukaguzi kuhusu mwongozo wa usimamizi wa vihatarishi na udhibiti wa ndani katika taasisi za umma na kuwajengea uwezo waratibu wa usimamizi wa vihatarishi kuhusu mwongozo wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma.

Amesema, hadi Aprili 2024, wizara imefanikiwa kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani 64 kuhusu viwango vya kitaaluma vya kimataifa vya ukaguzi wa mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha za umma.

Pia, kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani 80 kuhusu matumizi ya mfumo wa GIA-MIS, kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani 724 katika ukaguzi wa taarifa za fedha na kufanya tathmini ya ubora wa ukaguzi kwa taasisi 140.

"Katika kipindi hicho, wizara imefanya tathmini ya mifumo ya udhibiti wa ndani kwa vitengo vya ukaguzi wa ndani katika halmashauri 22 za mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Manyara.

"Vilevile, wizara imetoa mafunzo 14 kwa kamati za ukaguzi katika taasisi za umma 17 pamoja na waratibu wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi 51.

"Hadi Aprili 2024, wizara imefanikiwa kufanya kaguzi maalumu sita ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa mapato na matumizi ya fedha za umma."

Amesema, maeneo yaliyohusika na kaguzi hizo ni Mfumo wa Usimamizi wa Mapato ya VIZA, malimbikizo ya pensheni kwa wastaafu, madai ya mifuko ya hifadhi ya jamii na Shirika la Taifa la Bima (NIC), ruzuku kwa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) na akaunti za mirathi katika mahakama.

"Kaguzi nyingine za kimkakati zilizofanyika ni Mradi wa Barabara ya Mabasi Yaendayokasi Awamu ya 4 na 5 katika mkoa wa Dar es Salaam na ufanisi wa miradi nane ya kimkakati katika halmashauri sita Tanzania Bara."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news