Zanzibar, Saudi Arabia zakubaliana shughuli za Hijja

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, tayari imekubaliana na Serikali ya Saudi Arabia ya kuwa na akaunti mbili za uendeshaji wa shughuli za Hijja chini ya Ofisi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, imeeleza imekubaliana na Shirika la Ndege la Saudi Arabia kunza safari za moja kwa moja ifikapo mwakani hadi uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ili kuwapa wepesi Mahujaji wa Zanzibar kusafiri na kwa gharama nafuu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Juni 17,2024 Viwanja za maeneo huru ya Uwekezaji Mziwa Ng’ombe, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini, Pemba alipozungumza kwenye Baraza la Eid Hajj.
Al hajj Dkt. Mwinyi alisema, Hijja ni mfano wa taasisi ya mafunzo na malezi ya maarifa kwa Waislamu, pia ni ina mchango muhimu kwa mja kuwa mcha Mungu na kujiepusha na vitendo vyote viovu.

Akizungumzia utekelezaji wa dhamira ya Serikali juu ya uanzishaji wa Mfuko wa maalum wa Hijja nchini, Al hajj Dkt. Mwinyi alisema mfuko huo utawasaidia waislamu wengi kwenda kutekeleza ibada ya hiyo.
Pia alieleza tayari Serikali ya Mapinduzi imepokea ripoti ya Kamati ya wataalamu ya kuimarisha Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ili iendeshwe kwa ufanisi na kuleta tija zaidi ikiwemo kuanzisha na kusimamia Mfuko wa Hijja nchini ambapo mapendekezo ya ripoti hiyo yamezingatia upeo mkubwa wa shughuli za taasisi hiyo ikiwemo uanzishaji na usimamizi wa Mfuko wa Hijja, usimamizi wa fedha za Zakka na uratibu wa Baytul mali, umra na ziara kwenye maeneo ya historia ya Uislamu au utalii wa Kiislamu.
Mapema kabla ya Baraza la Eid, Al hajj Dk. Mwinyi alishiriki ibada ya kuchinja mara baada ya sala ya Eid na baadae alizungumza na Masheikh, viongozi wa dini na Maulamaa pamoja na kuwapa mkono wa Eid el Adhha watu wa makundi maalum, wakiwemo Wazee, wajane, watoto yatima, wenye ulemavu na mahitaji maalumu.

Al hajj Dk. Mwinyi alizishukuru Ofisi za mufti na ya kadhi Zanzibar, kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kusimamia na kuratibu masuala ya dini nchini.
Halikadhalika, Al hajj Dkt. Mwinyi, aliliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa na Wilaya pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuimarisha usalama kwenye maeneo yote pamoja na kusimamia usalama barabarani hasa kipindi hiki cha siku kuu ya Eid Adhha.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman, amezishukuru kamati za kitaifa zilizosimamia shughuli yote hadi kufanikishwa kwa sala ya Eid kitaifa na Baraza la Eid.
Mapema, kwenye ibada ya Sala ya Eid, Khatibu wa Sala hiyo alieleza umuhimu wa ushirikiano, umoja na mshikano baina ya Waislam na kuwataka kuendelea kuwa kitu kimoja katika kumuabudu Allah (S.W) akinasibisha na tukio la Hijja la Makka, Saudi Arabia ambako Mahujaji wote hukaa sehemu moja wakifanya matendo mamoja pamoja na kuvaa vazi moja bila ya kujali tofauti za utaifa wao, jinsia, rangi, kabila wala tofauti za vipato vyao.
Jumla ya Mahujaji 2087 kati ya 3300 kwa mwaka huu kutoka Tanzania walikwenda Makka Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hijja, huku ikielezwa idadi kutoka Zanzibar kongezeka ikilinganisha na idadi ya Mahujaji waliohiji mwaka jana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news