IRINGA-Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amewataka viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuepuka kutoa kauli au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.

Balozi Nchimbi amesema hayo akiwa Chuo cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Ihemi, mkoani Iringa, alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa jumuiya hiyo wa ngazi za mikoa na wilaya zote, nchi nzima, leo Julai 11,2024.
“Suala jingine ninataka kuwasisitiza UVCCM ni umuhimu wa watendaji wetu, viongozi wetu na wanachama wetu kutambua kuwa mnabeba taswira ya chama chetu kila wakati, katika mnayosema au kutenda. Kama kuna jambo tunapaswa kulilinda kwa wivu mkubwa ni taswira chanya ya CCM, hasa jambo linalohusu dhamana ya kuongoza nchi yetu na kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa, kwa kupinga kauli na vitendo vya ubaguzi na dhuluma kwa Watanzania,” amesema Balozi Nchimbi na kuongeza;

Aidha, katika kulinda dhima hiyo ya CCM, Balozi Nchimbi amewakumbusha wana-CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa hadi sasa hakuna chama kingine tofauti na CCM kimeonesha uwezo wa kuongoza nchi na pia wananchi hawako tayari kufanya majaribio kwa vyama vingine ambavyo havina mwelekeo, hali ambayo ni hatari kwa uimara wa nchi.


Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Komredi Joketi Urban Mwegelo akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya mafunzo hayo, amesema yatawasaidia viongozi na watendaji wa jumuiya hiyo kwenye mikoa, wilaya na hatimae kushuka ngazi zingine nchi nzima kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi unaohitajika.