DAR-Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji,Mheshimiwa Phaustine Kasike amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Ephraim Balozi Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB).Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Maputo,Msumbiji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,katika mkutano huo, Bw. Mafuru amemueleza Balozi Kasike kwamba katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, TTB imeamua kufanya kazi kwa ukaribu na taasisi mbalimbali ikiwemo Balozi za Tanzania nje ya nchi ili kuongeza idadi ya watalii kutoka nje.
Hivyo, amemuomba Balozi Kasike kuipatia ofisi yake malengo na mikakati ya Ubalozi katika kuiwezesha Tanzania kunufaika na Sekta ya Utalii ili kuweka mikakati ya pamoja kwa maslahi ya nchi.
Mhe. Balozi ameahidi kutoa kila aina ya ushirikiano kwa TTB ili Taasisi hiyo iweze kufikia malengo yake.
Aidha, ameahidi kuiunganisha taasisi hiyo na taasisi zinazohusika na Sekta ya Utalii ili kuangalia uwezekano wa kuwa na mashirikiano.