DAR-Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji,Mheshimiwa Phaustine Kasike amekutana na Bw. John Mathew Mbali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mkutano huo umefanyika kwenye ofisi za TIC zilizopo Posta jijini Dar es Salaam ambapo viongozi hao wamejadiliana kuhusu kufanya kazi kwa ukaribu ili kuwafikia wadau wa biashara na uwekezaji kutoka Msumbiji ili kuja kuwekeza Tanzania.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji.
Aidha, viongozi hao wamekubaliana kuanzia sasa kuzishawishi mamlaka na wadau wengine wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Msumbiji kushiriki katika matukio mbalimbali ya kibiashara yanayofanyika katika nchi hizi ili kupata fursa ya kutangaza bidhaa na huduma wanazotoa kwa lengo la kupata masoko.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Kasike ameeleza kwamba katika Utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi, moja ya Jukumu la Msingi la Ubalozi ni kuziunganisha taasisi na wadau wengine wa Sekta ya Biashara na Uwekezaji kutoka Tanzania.
Pia,kufanya kazi kwa ukaribu na wenzao wa Msumbiji kwa maslahi ya nchi zetu mbili. Hivyo, aliahidi kutoa kila aina ya ushirikiano katika kutekeleza jukumu hilo.